The Book of Common Prayer
United States England Scotland Ireland Wales Canada World

    Kitabu cha Sala za Kanuni (1918)
The Zanzibar Book of Common Prayer in Swahili

 

SALA ZA KUOMBEA WAFU

Siku ya Ukumbusho wa Roho zote kila Antifona isemwe nzima mwanzo na mwisho wa Zaburi.

Siku yo yote ikisemwa sala hii peke yake, wala si mara baada ya Sala ya Jioni ya siku ile, zisemwe kwanza sala za siri ilivyo kawaida.

Siku yo yote ikisemwa sala hii mara baada ya Sala ya Jioni ya siku ile, mwisho wa Sala ya Jioni ya siku isisemwe, Roho zao waaminifu, etc. bali mara hufuata Sala ya Jioni ya Wafu.
 

Prayers for Commemorations of the Departed

Sala ya Jioni

Inaanzia ZABURI.

    Ant. Nitaenenda mbele za BWANA Katika nchi za wahai.
 

Evening Prayer

ZAB. 116

1. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza *
    Sauti yangu na dua zangu.
2. Kwa maana amenitegea sikio lake, *
    Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.
3. Kamba za mauti zilinizunguka; *
    Shida za kuzimu zilinipata.
4. Naliona taabu na huzuni; *
    Nikaliitia Jina la BWANA.

5. Ee BWANA, nakuomba sana, *
    Uniokoe nafsi yangu.
6. BWANA yu mwenye neema na haki, *
    Naam, Mungu wetu yu mwenye rehema.
7. BWANA huwalinda wasio na hila; *
    Nalidhilika akaniokoa.
8. Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako, *
    Kwa kuwa BWANA amekutendea ukarimu.
9· Maana umeniponya nafsi yangu na mauti, macho yangu na machozi, *
    Na miguu yangu na kuanguka.
10. Nitaenenda mbele za BWANA *
    Katika nchi za wahai.

Raha ya milele *
    Uwajalie, Ee BWANA.
Na nuru ya daima *
    Iwaangaze.

    Ant. Nitaenenda mbele za BWANA Katika nchi za wahai.
    Ant. Ole wangu mimi, Ee BWANA! Kwa kuwa kukaa kwangu kumezidishwa.
 

Psalm 116

ZAB. 120

1. Katika shida yangu nalimlilia BWANA, *
    Naye akaniitikia.
2. Ee BWANA, uniponye nafsi yangu, *
    Na midomo ya uongo na ulimi wa hila.
3. Akupe nini, akuzidishie nini, *
    Ewe ulimi wenye hila?
4. Mishale ya mtu hodari iliyochongoka, *
    Pamoja na makaa ya mretemu.
5. Ole wangu mimi! *
    Kwa kuwa nimekaa katika Mesheki.
6. Na kufanya maskani yangu *
    Katikati ya hema za Kedari.
7. Nafsi yangu nimekaa siku nyingi *
    Pamoja naye aichukiaye amani.
8. Mimi ni wa amani, *
    Bali ninenapo wao huelekea vita.

    Raha ya milele.

    Ant. Ole wangu mimi, Ee BWANA! Kwa kuwa kukaa kwangu kumezidishwa.
    Ant. Bwana atakulinda na mabaya yote, BWANA atakulinda nafsi yako.
 

Psalm 120

ZAB. 121

1. Nitayainua macho yangu niitazame milima; *
    Msaada wangu utatoka wapi?
2. Msaada wangu u katika BWANA, *
    Aliyezifanya mbingu na nchi.
3. Asiache mguu wako usogezwe; *
    Asisinzie akulindaye.
4. Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, *
    Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
5. BWANA ndiye mlinzi wako; *
    BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume.
6. Jua halitakupiga mchana, *
    Wala mwezi wakati wa usiku.
7. BWANA atakulinda na mabaya yote, *
    Atakulinda nafsi yako.
8. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, *
    Tangu sasa na hata milele.

    Raha ya milele.

    Ant. BWANA atakulinda na mabaya yote, BWANA atakulinda nafsi yako.
    Ant. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
 

 

ZAB. 130

1. BWANA, toka vilindini nimekulilia, *
    Ee Bwana, uisikie sauti yangu.
2. Masikio yako na yaisikilize *
    Sauti ya dua zangu.
3. BWANA, kama Wewe ungehesabu maovu, *
    Ee Bwana, nani angesimama?
4. Lakini kwako kuna msamaha, *
    Ili Wewe uogopwe.
5. Nimemngoja BWANA, roho yangu imengoja, *
    Na neno lake nimelitumainia.
6. Nafsi yangu ninamngoja Bwana, *
    Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi.
7. Ee Israeli, umtarajie BWANA; *
    Madhali kwa BWANA kuna fadhili.
8. Na kwake kuna ukombozi mwingi; *
    Atamkomboa Israeli na maovu yake yote.

    Raha ya milele.

    Ant. BWANA, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
    Ant. Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.
 

Psalm 130

ZAB. 138

1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote; *
    Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
2. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu; *
    Nitalishukuru Jina lako.
3. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, *
    Kwa maana umelikuza Jina lako juu ya yote.
4. Siku ile niliyokuita uliniitikia; *
    Ukanifariji nafsi yangu kwa kunitia nguvu.
5 . BWANA, wafalme wote wa dunia watakushukuru, *
    Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
6. Naam, wataziimba njia za BWANA, *
    Kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu.
7. Ingawa BWANA yuko juu amwona mnyenyekevu, *
    Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
8. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha; *
    Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui.
9. Na mkono wako wa kuume utaniokoa; *
    BWANA atanitimilizia mambo yangu.
10. Fadhili zako, BWANA, ni za milele; *
    Usiziache kazi za mikono yako.

    Raha ya milele.

    Ant. Ee BWANA, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.

SOMO na WIMBO hapana.

V. Nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema.
R. Wa heri wafu wafao katika BWANA.

    Ant. Mag. Wote anipao Baba watakuja kwangu, wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.

MAGNIFICAT, na mwishoni, Raha ya milele.

Ikiisha MAGNIFICAT na Antifona yake, wote wapige magoti; na mara hufuata,

    Baba yetu (kimoyomoyo).
    V. Usitutie majaribuni.
    R. Lakini utuokoe na yule mwovu.
 † V. Ee BWANA, uziokoe roho zao.
    R. Na milango ya Jehanum.
    V. Wastarehe katika amani.
    R. Amin.
    V. Ee BWANA, usikie kuomba kwetu.
    R. Kilio chetu kikufikie.
    V. BWANA akae nanyi.
    R. Pia na roho yako.
 

Psalm 138

 

Ikisemwa sala hii kwa ajili ya mtu mmoja.

    V. Ee BWANA, uiokoe roho yake.
    R. Na milango ya Jehanum.
    V. Astarehe katika amani.
    R. Amin.

Walakini isitumike jumla ya umoja mahali pengine.

Tuombe

Ee Mungu, umewaumba waaminifu wote na kuwaokoa: Uzijalie roho za watumishi na wajakazi wako ondoleo la dhambi zao zote; wapewe, kwa sala za pendo, masamaha waliyoyataka sikuzote. Uishiye na kumiliki pamoja na Mungu Baba, katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu daima milele na milele. Amin.

V. BWANA akae nanyi.
R. Pia na roho yako.
V. Raha ya milele uwajalie, Ee BWANA.
R. Na nuru ya daima iwaangaze.
Wastarehe katika amani.
R. Amin.

Ni halali kusema sala hii mara moja kwa mwezi kutangulia Missa ya Wafu ya kwanza ya mwezi; yaani isemwe jioni panapo Missa ya Wafu asubuhi ifuatayo.

Na vile vile mara moja kwa juma Wakati wa Majilio na Kwaresima.

Walakini Antifona zisisemwe nzima mbele ya Zaburi wala mbele ya Magnificat, ila hata mwisho wa italics tu.

Aidha, yafaa kusema sala hii kwa ajili ya mtu fulani siku ya kufa kwake, au kuzikwa kwake, au siku ya ukumbusho wake; au kwa ajili ya watu fulani vile vile.

Tena, ikiwa hivyo, Antifona na zisemwe nzima mwanzo na mwisho wa Zaburi na Magnificat, walakini Sala na ibadiliwe hivi,
 

 

(1) Askofu au Kasisi

Ee Mungu, ulimkubali mtumishi wako N. kuwa Askofu (au Kasisi) wa Mwana wako: Usikie kuomba kwetu; umjalie furaha ya milele pamoja na Maaskofu (au Makasisi) wako waaminifu. Kwa Yeye.
 

Bishop or Priest

(2) Siku ya kufa au ya kuzikwa

Ee Bwana, tunakuomba, uighofiri roho ya mtumishi wako N. aliyeifariki dunia ili akuishie Wewe: Umsamehe yote aliyokukosa kwa udhaifu wake wa ubinadamu; na kumsafisha kwa huruma zako nyingi. Kwa.
 

Day of death or burial

(3) Siku ya ukumbusho

Ee Mungu, Bwana wa rehema: Tunawaombea kwako watumishi wako N. na N. ambao tunawakumbuka mbele zako leo; uwajalie mahali pa kuburudika, furaha ya amani, na mwanga wa nuru yako. Kwa.

Siku ya Ukumbusho wa Roho zote na zisemwe sala hizi zifutazo, lakini siku nyingine zisisemwe.
 

Memorial day

Sala ya Usiku (ya Nov. 1-2)

Naungama, nk.
Mwenyezi Mungu, nk.
Bwana Mwenyezi, nk.

    ZABURI pasipo Antifona, na mwishoni, Raha ya milele.

    NUNC DIMITIIS pasipo Antifona, na mwishoni, Raha ya milele.

Ikiisha NUNC DIMITTIS, wapige magoti, waseme, Baba yetu, etc. kama sala ya jioni, isipokuwa,

Sala

Ee Bwana, tunakusihi: Uwahurumie roho za watumishi wako tunaowaombea kwako uliye Mtukufu; uzikubali dua zetu za upendo na unyenyekevu, ili wastahili kuifikia raha ya milele. Kwa.
 

Night Prayer

Sala ya Asubuhi (ya Nov. 2)

Inaanzia (zikiisha sala za siri).

VENITE, na mwishoni, Raha ya milele.

Ndipo hufuata ZABURI.

    Ant. Mifupa uliyoiponda Na imfurahie BWANA.
 

Morning Prayer

ZAB. 51

1. Ee Mungu, unirehemu, *
    Sawasawa na fadhili zako.
2. Kiasi cha wingi wa rehema zako *
    Uyafute makosa yangu.
3. Unioshe kabisa na uovu wangu; *
    Unitakase dhambi zangu .
4. Maana nimejua mimi makosa yangu, *
    Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
5. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, *
    Na kufanya maovu mbele za macho yako.
6. Wewe ujulike kuwa una haki unenapo, *
    Na kuwa safi utoapo hukumu.

7. Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; *
    Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
8. Bali wapendezwa na kweli iliyo moyoni; *
    Nawe utanijulisha hekima kwa siri.
9. Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi; *
    Unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
10. Unisikize furaha na shangwe, *
    Mifupa uliyoiponda ifurahi.
11. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; *
    Uzifute hatia zangu zote.

12. Ee Mungu, uniumbie moyo safi; *
    Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
13. Usinitenge na uso wako; *
    Wala Roho wako Mtakatifu usiniondolee.
14. Unirudishie furaha ya wokovu wako; *
    Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
15. Nitawafundisha wakosaji njia zako, *
    Na wenye dhambi watarejea kwako.
16. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, uniponye na damu za watu, *
    Na ulimi wangu utaiimba haki yako.

17. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, *
    Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
18. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, *
    Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
19. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; *
    Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.
20. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako; *
    Uzijenge kuta za Yerusalemu.
21. Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, *
    Na sadaka za kuteketezwa na kafara.
22. Ndipo watakapotoa ng'ombe *
    Juu ya madhabahu yako.

    Raha ya milele.

    Ant. Mifupa uliyoiponda Na imfurahie BWANA.
    Ant. Wewe, BWANA, usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.
 

Psalm 51

ZAB. 65

1. Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, *
    Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.
2. Wewe usikiaye kuomba, *
    Wote wenye mwili watakujia.
3. Ingawa maovu mengi yanatushinda, *
    Wewe utayafunika maasi yetu.

4. Yu heri mtu yule umchaguaye, *
    Na kumkaribisha akae nyuani mwako.
5. Na tushibe wema wa nyumba yako, *
    Patakatifu pa hekalu lako.
6. Kwa mambo ya kutisha utatujibu, *
    Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu.
7. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, *
    Na la bahari iliyo mbali sana.
8. Milima waiweka imara kwa nguvu zako, *
    Huku ukijifunga uweza kama mshipi.
9. Wautuliza uvumi wa bahari, *
    Uvumi wa mawimbi yake, na ghasia ya mataifa.

10. Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; *
    Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.
11. Umeijilia nchi na kuisitawisha; *
    Umeitajirisha sana.
12. Mto wa Mungu umejaa maji;
    Wawaruzuku watu nafaka.
13. Maana ndiwe uitengenezaye ardhi; *
    Matuta yake wayajaza maji.
14. Wapasawazisha palipoinuka; *
    Wailainisha nchi kwa manyunyu
15. Waibariki mimea yake; *
    Umeuvika mwaka taji ya wema wako.

16. Mapito yako yadondoza unono; *
    Huyadondokea malisho ya nyikani.
17. Na vilima vyajifunga furaha; *
    Na malisho yamevikwa kondoo;
18. Na mabonde yamepambwa nafaka; *
    Yanashangilia, naam, yanaimba.

    Raha ya milele.

    Ant. Wewe, BWANA, usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.
    Ant. Katika malisho ya majani mabichi BWANA hunilaza.
 

 
Psalm 65

ZAB. 23

1. BWANA ndiye mchungaji wangu, *
    Sitapungukiwa na kitu.
2. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza; *
    Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

3. Hunihuisha nafsi yangu na kuniongoza, *
    Katika njia za haki kwa ajili ya Jina lake.
4. Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, *
    Sitaogopa mabaya.

5. Kwa maana Wewe upo pamoja nami; *
    Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
6. Waandaa meza mbele yangu, *
    Machoni pa watesi wangu.

7. Umenipaka mafuta kichwani pangu, *
    Na kikombe changu kinafurika,
8. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; *
    Nami nitakaa nvumbani mwa BWANA milele.

    Raha ya milele.

    Ant. Katika malisho ya majani mabichi BWANA hunilaza.
    Ant. Kila mwenye pumzi Na amsifu BWANA.
 

Psalm 23

ZAB. 150

1. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; *
    Msifuni katika anga la uweza wake.
2. Msifuni kwa matendo yake makuu; *
    Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
3. Msifuni kwa mvumo wa baragumu; *
    Msifuni kwa kinanda na kinubi.
4. Msifuni kwa matari na kucheza; *
    Msifuni kwa zeze na filimbi.
5. Msifuni kwa matoazi yaliayo; *
    Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA; *
    Msifuni BWANA.

    Raha ya milele.

Ant. Kila mwenye pumzi Na amsifu BWANA.
SOMO LA KWANZA. Hekima iii; 1-9 (313A).

Leo mwisho wa Masomo, Msomaji asikibusu kitabu wala isisemwe, V. Nawe, BWANA, uturehemu.

   Ant. Ee BWANA, uiokoe roho yangu Na milango ya Jehanum.
    EGO DIXI, na mwishoni, Raha ya milele. (uk. 6)
    SOMO LA PILI. Ufunuo vi; 9-11.

    V. Ee BWANA, uniokoe na mauti ya milele, kunako siku ile ya hofu; * mbingu na nchi zitakapotikisika; * utakapokuja kuuhukumu ulimwengu kwa moto.
    R. Ee BWANA, uniokoe, etc.
    V. Nimeingiwa na hofu, ninatetemeka; * hata hukumu iwekwe, ghadhabu ikaonekane.
    R. Mbingu na nchi * zitakapotikisika.
    V. Siku ile ya ghadhabu, shida, na huzuni; * siku ya uchungu mwingi.
    R. Utakapokuja * kuuhukumu ulimwengu kwa moto.
    V. Raha ya milele uwajalie, Ee BWANA; * na nuru ya daima iwaangaze.
    R. Ee BWANA, uniokoe, etc.

    WIMBO hapana.

V. Nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema.
R. Wa heri wafu wafao katika BWANA.

    Ant. Ben. Mimi ndimi ufufuo, na uzima, yeye aniaminiye Mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; Naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.

    BENEDICTUS, na mwishoni, Raha ya milele.

Ikiisha BENEDICTUS na Antifona yake, wapige magoti, waseme, Baba yetu, etc. kama sala ya jioni.

Sala ya Adhuhuriya Nov. 2 ndiyo ya Oktavo ya Watakatifu wote.
 


 

Psalm 150

KUJIWEKA TAYARI KABLA YA MISSA

    Ant. Ee BWANA, usiyakumbuke makosa yetu, wala makosa ya baba zetu; wala usitupatilize kwa dhambi zetu. (W. P. Haleluya).
 

Preparation before the Mass

ZAB. 84

1. Maskani zako zapendeza kama nini,
    Ee BWANA wa majeshi!
2. Nafsi yangu nimezionea shauku nyua za BWANA,
    Naam, na kuzikondea,
3. Moyo wangu na mwili wangu
    Vinamlilia Mungu aliye hai.
4. Shomoro naye amejipatia nyumba,
    Na mbayuwayu kioto alipoweka makinda yake;
5. Kwenye madhabahu zako, BWANA wa majeshi,
    Mfalme wangu na Mungu wangu.
6. Wa heri wakaao nyumbani mwako;
    Wanakuhimidi daima.

7. Yu heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
    Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
8. Wakilipitia bonde la Vilio hulifanya chemchemi;
    Naam, mvua ya vuli hulivika baraka.
9. Huendelea toka nguvu hata nguvu;
    Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
10. BWANA Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu
    Ee Mungu wa Yakobo, usikilize.

11. Ee Mungu, ngao yetu, uangalie,
    Umtazame uso Masihi wako.
12. Hakika siku moja katika nyua zako
    Ni bora kuliko siku elfu.
13. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu
    Kuliko kukaa katika hema za uovu.
14. Kwa kuwa BWANA Mungu ni jua na ngao;
    BWANA atatoa neema na utukufu;
15. Hatawanyima kitu chema
    Hao waendao kwa ukamilifu.
16. Ee BWANA wa majeshi,
    Yu heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.
    Atukuzwe.
 

Psalm 84

ZAB. 85

1. BWANA, umeiridhia nchi yako,
    Umewarejeza mateka wa Yakobo.
2. Umeusamehe uovu wa watu wako,
    Umezisitiri hatia zao zote.
3. Umeiondoa ghadhabu yako yote,
    Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.
4. Ee Mungu wa wokovu wetu, uturudishe,
    Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.

5. Je! utatufanyia hasira hata milele?
    Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi?
6. Je! hutaki kurudi na kumhuisha,
    Watu wako wakufurahie?
7. Ee BWANA, utuonyeshe rehema zako,
    Utupe wokovu wako.

8. Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA,
    Maana atawaambia watu wake amani;
9. Naam, na watauwa wake pia;
    Bali wasiurudie upumbavu tena.
10. Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
    Utukufu ukae katika nchi yetu.

11. Fadhili na kweli zimekutana;
    Haki na amani zimebusiana;
12. Kweli imechipuka katika nchi;
    Haki imechungulia kutoka mbinguni.
13. Naam, BWANA atatoa kilicho chema,
    Na nchi yetu itatoa mazao yake.
14. Haki itakwenda mbele zake,
    Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
    Atukuzwe.
 

Psalm 85

ZAB. 86

1. Ee BWANA, utege sikio lako uniitikie,
    Maana mimi ni maskini na mhitaji.
2. Unihifadhi nafsi yangu,
    Maana mimi ni mtu mtauwa.
3. Wewe uliye Mungu wangu,
    Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
4. Wewe, Bwana, unifadhili,
    Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
5. Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
    Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
6. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
    Umekuwa tayari kusamehe;
7. Na mwingi wa fadhili
    Kwa watu wote wakuitao.

8. Ee BWANA, uyasikie maombi yangu;
    Uisikilize sauti ya dua zangu.
9. Siku ya mateso yangu nitakuita,
    Kwa maana utaniitikia.
10. Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana,
    Wala matendo mfano wa matendo yako.
11. Mataifa yote uliowafanya watakuja;
    Watakusujudia Wewe, Bwana;
12. Watalitukuza Jina lako,
    Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu.

13. Wewe ndiwe mfanya miujiza,
    Ndiwe Mungu peke yako.
14. Ee BWANA, unifundishe njia yako;
    Nitakwenda katika kweli yako.
15. Uniunge moyo wangu na kicho cha Jina lako;
    Nitakusifu Wewe, Bwana.
16. Mungu wangu, kwa moyo wangu wote
    Nitalitukuza Jina lako milele.
17. Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana;
    Umeniopoa nafsi yangu na kuzimu.

18. Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia;
    Mkutano wa wakatili wamenitafuta;
19. Wala hawakukuweka Wewe, Bwana,
    Mbele ya macho yao.
20. Lakini Wewe, Bwana,
    U Mungu wa rehema na neema;
21. Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli;
    Unielekee na kunifadhili mimi.
22. Mpe mtumishi wako nguvu zako;
    Umwokoe mwana wa mjakazi wako;
23. Unifanyie ishara ya wema;
    Wanichukiao waione na kuaibishwa.
24. Kwa kuwa Wewe, Bwana,
    Umenisaidia na kunifariji.
    Atukuzwe.
 

Psalm 86

ZAB. 116

11. Naliamini, kwa maana nitanena,
    Mimi naliteswa sana;
12. Mimi nalisema kwa haraka yangu,
    Wanadamu wote ni waongo.
13. Nimrudishie BWANA nini
    Kwa ukarimu wake wote alionitendea ?
14. Nitakipokea kikombe cha wokovu,
    Na kulitangaza Jina la BWANA.
15. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA,
    Naam, mbele ya watu wake wote.
16. Ina thamani machoni pa BWANA
    Mauti ya watauwa wake.

17. BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako;
    Umevifungua vifungo vyangu.
18. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru,
    Na kulitangaza Jina la BWANA.
19. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA,
    Naam, mbele ya watu wake wote.
20. Katika nyua za nyumba ya BWANA,
    Ndani yako, Ee Yerusalemu.
    Atukuzwe.
 

Psalm 116

ZAB. 130

1. BWANA, toka vilindini nimekulilia,
    Ee Bwana, uisikie sauti yangu.
2. Masikio yako na yaisikilize
    Sauti ya dua zangu.

3. BWANA, kama Wewe ungehesabu maovu,
    Ee Bwana, nani angesimama ?
4. Lakini kwako kuna msamaha,
    Ili Wewe uogopwe.

5. Nimemngoja BWANA, roho yangu imengoja,
    Na neno lake nimelitumainia.
6. Nafsi yangu ninamngoja Bwana
    Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi.

7. Ee Israeli, umtarajie BWANA;
    Madhali kwa BWANA kuna fadhili.
8. Na kwake kuna ukombozi mwingi;
    Atamkomboa Israeli na maovu yake yote.
    Atukuzwe.

    Ant. Ee BWANA, usiyakumbuke makosa yetu, wala makosa ya baba zetu; wala usitupatilize kwa dhambi zetu. (W. P. Haleluya).

Bwana, uturehemu.
    Kristo, uturehemu.
Bwana, uturehemu.

Baba yetu (kimoyomoyo).
V. Usitutie majaribuni.
R. Lakini utuokoe na yule mwovu.
V. Nalisema, Ee BWANA, unifadhili,
R. Uniponye, maana nimekutenda dhambi.
V. Ee BWANA, urudi; hata lini?
R. Uwahurumie watumishi wako.
V. Ee BWANA, fadhili zako zikae nasi.
R. Kama vile tulivyokungoja Wewe.
V. Makuhani wako na wavikwe haki.
R. Watauwa wako na washangilie.
V. Unitakase na mambo ya siri.
R. Unizuie nisitende mambo ya kiburi.
V. Ee BWANA, usikie kuomba kwetu.
R. Kilio chetu kikufikie.
V. BWANA akae nanyi.
R. Pia na roho yako.

Tuombe

    Ee Mungu mwenye neema, uyatege masikio yako ya rehema kwa sala zetu, na kututia nuru mioyoni mwetu kwa neema ya Roho Mtakatifu; ili tuzihudumie siri zako takatifu kama itupasavyo, na kukupenda kwa pendo la milele.
    Ee Bwana, utuchome moto wa Roho Mtakatifu viuno ni na mioyoni; ili tukutumikie wenye miili safi, na kukupendeza wenye mioyo isiyo na mawaa.
    Ee Bwana, tunakusihi, huyu Msaidizi atokaye kwako atuangaze nia zetu; na, kama Mwanao alivyoahidi, atuongoze katika kweli yote.
    Ee Bwana, tunakusihi, uweza wa Roho Mtakatifu utushukie; ili kwa rehema zake atutakase mioyo yetu, na kutulinda na mabaya yote.
    Ee Mungu, uliwafundisha mioyo yao wenye imani kwa nuru ya Roho Mtakatifu; utujalie kwa Roho huyo tuyajue mambo yote kwa akili, na kuifurahia sikuzote faraja yake takatifu.
    Ee Bwana, tunakusihi, uje utusafishe dhamiri zetu; ili, ajapo Bwana wetu Yesu Kristo Mwana wako, aone ndani yetu makao yaliyoandaliwa tayari. Aishiye na kumiliki pamoja nawe, katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu daima milele na milele. Amin.

 

Psalm 130

KUSHUKURU BAADA YA MISSA

    Ant. Tuimbe wimbo wa vijana watatu, waliouimba katika tanuu la moto; wakamhimidi BWANA. (W. P. Haleluya).
 

Thanksgiving after the Mass

BENEDICITE.   Dan. iii

1. Enyi viumbe vyote vya BWANA, mhimidini BWANA;
    Msifuni na kumwadhimisha milele.
2. Malaika za BWANA, mhimidini BWANA;
    Mbingu na zimhimidi BWANA;
3. Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini BWANA;
    Mawezo yote ya BWANA, mhimidini BWANA;
4. Jua na mwezi, mhimidini BWANA;
    Nyota za mbinguni, mhimidini BWANA;
5. Manyunyu yote na ukungu, mhimidini BWANA;
    Pepo zote za Mungu, mhimidini BWANA;
6. Moto na hari, mhimidini BWANA;
    Kipupwe na musimu, mhimidini BWANA;
7. Umande na sakitu, mhimidini BWANA;
    Jalidi na baridi, mhimidini BWANA;
8. Barafu na theluji, mhimidini BWANA;
    Usiku na mchana, mhimidini BWANA;
9. Weupe na giza, mhimidini BWANA;
    Umeme na mawingu, mhimidini BWANA;

10. Dunia na imhimidi BWANA;
    Imsifu na kumwadhimisha milele.
11. Milima na vilima, mhimidini BWANA;
    Mimea yote ya nchi, mhimidini BWANA;
12. Chemchemi, mhimidini BWANA;
    Bahari na mito, mhimidini BWANA;
13. Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini BWANA;
    Ndege zote za angani, mhimidini BWANA;
14. Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini BWANA;
    Wanadamu, mhimidini BWANA;
15. Bani Israeli, mhimidini BWANA;
    Msifuni na kumwadhimisha milele.
16. Makuhani wa BWANA, mhimidini BWANA;,
    Watumishi wa BWANA, mhimidini BWANA;
17. Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini BWANA;
    Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini BWANA;
18. Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini BWANA;
    Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumhimidi Baba na Mwana na Roho Mtakatifu;
    Tumsifu na kumwadhimisha milele.
Ee BWANA, umehimidiwa katika anga la mbinguni;
    Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
 

 

ZAB. 150

1. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; *
    Msifuni katika anga la uweza wake.
2. Msifuni kwa matendo yake makuu; *
    Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
3. Msifuni kwa mvumo wa baragumu; *
    Msifuni kwa kinanda na kinubi.
4. Msifuni kwa matari na kucheza; *
    Msifuni kwa zeze na filimbi.
5. Msifuni kwa matoazi yaliayo; *
    Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA; *
    Msifuni BWANA.
    Atukuzwe.

    Ant. Tuimbe wimbo wa vijana watatu, waliouimba katika tanuu la moto; wakamhimidi BWANA. (W. P. Haleluya).

Bwana, uturehemu.
    Kristo, uturehemu.
Bwana, uturehemu.

Baba yetu (kimoyomoyo).
V. Usitutie majaribuni.
R. Lakini utuokoe na yule mwovu.
V. BWANA, kazi zako zote zitakushukuru.
R. Na watauwa wako watakuhimidi.
V. Watauwa na waushangilie utukufu.
R. Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
V. BWANA, kutukuza usitutukuze sisi.
R. Bali ulitukuze Jina lako.
V. Ee BWANA, usikie kuomba kwetu.
R. Kilio chetu kikufikie,
V. BWANA akae nanyi.
R. Pia na roho yako.

Tuombe

    Ee Mungu, uliwapunguzia wale vijana watatu ukali wa moto; utujalie kwa rehema zako, tusiteketezwe kwa moto wa dhambi zetu.
    Ee Bwana, tunakusihi, katika matendo yetu yote utuongoze kwa neema yako, na kutufanikisha daima kwa msaada wako; ili sala zetu zote na kazi zetu zianze kwako, na kwako zifulizwe na kumalizika.
    Ee Bwana, ulimpa Lorenzo Mtakatifu neema ya kustahimili maumivu ya moto na kushinda; utujalie, tunakusihi, tuizimishe miali ya tamaa zetu. Kwa Kristo Bwana wetu. Amin.
 


 

Psalm 150

IMANI IITWAYO YA ATHANASIO MT.

Isemwe pamoja na Antifona yake baada ya Zaburi za Sala ya Asubuhi Sikukuu hizi,

Ambrosio, Des. 7; Yohana Krisostomo, Jan. 27; Sirili wa Iskanderia, Feb. 9; Tomaso wa Akwino, Mar. 7; Leo, Apr. 11; Athanasio, Mei. 2; Basileo, Jun. 14; Bonaventura, Jul. 14; Agostino wa Hipo, Ago. 28; Jerome, Sep. 30; Yakobo wa Yerusalemu, Okt. 23; na Klementi wa Rumi, Nov. 23.

    Ant. Hii ndiyo Imani Katholiko; Ambayo kwamba kila atakaye kuokoka imempasa kuishika.
    1. Kila atakaye kuokoka, * Zaidi ya yote imempasa kuishika Imani Katholiko.
    2. Nayo asipoihifadhi kamili na safi, * Bila shaka atapotea milele.
    3. Na Imani Katholiko ni hii; * Tumwabudu Mungu mmoja katika Utatu, na Utatu katika Umoja.
    4. Tusizichanganye nafsi, * Wala kuugawanya Uungu
    5. Kwa maana nafsi ya Baba ni mbali, nafsi ya Mwana ni mbali, * Nafsi ya Roho Mtakatifu ni mbali.
    6. Walakini Uungu wa Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu ni Uungu mmoja, * Utukufu wao ni sawa, Ukuu wao ni wa milele.
    7. Kama alivyo Baba, ndivyo alivyo Mwana, * Ndivyo alivyo Roho Mtakatifu.
    8. Baba hakuumbwa, Mwana hakuumbwa, * Roho Mtakatifu hakuumbwa.
    9. Baba hana mpaka, Mwana hana mpaka, * Roho Mtakatifu hana mpaka.
    10. Baba ni wa milele, Mwana ni wa milele, * Roho Mtakatifu ni wa milele.
    11. Walakini hakuna watatu walio wa milele; * Bali aliye wa milele ni mmoja tu.
    12. Kadhalika hakuna watatu wasioumbwa, wala watatu wasio na mpaka; * Bali asiyeumbwa ni mmoja tu, na asiye na mpaka ni mmoja tu.
    13. Kadhalika Baba ni Mwenyezi, Mwana ni Mwenyezi, * Na Roho Mtakatifu ni Mwenyezi.
    14. Walakini hakuna watatu walio Wenyezi; * Bali aliye Mwenyezi ni mmoja tu.
    15. Vivyo hivyo Baba ni Mungu, na Mwana ni Mungu, * Na Roho Mtakatifu ni Mungu.
    16. Walakini hakuna Miungu watatu; * Bali aliye Mungu ni mmoja tu.
    17. Vivyo hivyo Baba ni Bwana, na Mwana ni Bwana, * Na Roho Mtakatifu ni Bwana.
    18. Walakini hakuna Bwana watatu; * Bali aliye Bwana ni mmoja tu.
    19. Kwa maana kama tunavyoshurutishwa kwa kanuni ya kweli ya Kikristo * Kukiri ya kuwa kila Nafsi ni Mungu na
wana;
    20. Kadhalika tunagombezwa na Imani Katholiko * Tusiseme ya kuwa wako Miungu watatu au Bwana watatu.
    21. Baba hakuumbwa na awaye yote; * Hakuhulukiwa, wala hakuzaliwa.
    22. Mwana anatoka katika Baba tu; * Hakuumbwa, wala hakuhulukiwa; bali yu Mwana wa azali.
    23. Roho Mtakatifu anatoka katika Baba na Mwana; * Hakuumbwa, wala hakuhulukiwa, wala hakuzaliwa; bali anatoka.
    24. Basi yupo Baba mmoja tu, si Baba watatu; yupo Mwana mmoja tu, si Wana watatu; * Yupo Roho Mtakatifu mmoja tu, si Roho Watakatifu watatu.
    25. Na katika Utatu huu hapana aliye wa kwanza na aliye wa baadaye; * Hapana aliye mkuu zaidi na aliye mdogo.
    26. Bali Nafsi zote tatu ni wa milele, * Wa sawa wote.
    27. Basi katika mambo yote kama tulivyokwisha kusema; * Imetupasa kuuabudu Umoja katika Utatu, na Utatu katika Umoja.
    28. Basi yeye atakaye kuokoka, * Na aone hivi juu ya Utatu.
    29. Na zaidi ya hayo, ili apate wokovu, * Imempasa kukuamini kwa moyo Kufanyika mwili kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
    30. Na Imani kamili ndiyo hii; * Tuamini na kukiri ya kuwa Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ni Mungu na Mwanadamu.
    31. Ni Mungu, ana Uungu wa Baba, yu Mwana wake wa azali; * Ni Mwanadamu, ana utu wa mama yake, alizaliwa katika zamani.
    32. Mungu kamili na Mwanadamu kamili; * Ana roho yenye akili na mwili wa kibinadamu.
    33. Yu sawa na Baba kwa kuwa ni Mungu; * Yu chini ya Baba kwa kuwa ni Mwanadamu.
    34. Na ijapokuwa yu Mungu na Mwanadamu, * Yeye si wawili, bali ni Kristo mmoja.
    35. Yeye ni mmoja, si kana kwamba Uungu umebadilika uwe mwili; * Bali kwa kuutwaa utu wa mwanadamu na kuuunga na Mungu.
    36. Mmoja kabisa; si kwa kuchanganyika Uungu na utu; * Bali kwa kuwa Nafsi mmoja tu.
    37. Kwa maana kama roho yenye akili pamoja na mwili huwa mwanadamu mmoja, * Kadhalika Mungu na Mwanadamu pamoja ni Kristo mmoja.
    38. Aliyeteswa kwa wokovu wetu, * Akashuka mahali pa wafu, akafufuka siku ya tatu.
    39. Akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba Mwenyezi, * Kutoka huko atakuja kuwahukumu wahai na wafu.
    40. Naye atakapokuja, wanadamu wote watafufuliwa na miili yao, * Watatoa habari za matendo yao.
    41. Nao waliotenda mema wataingia katika uzima wa milele; * Nao waliotenda mabaya katika moto wa milele.
    42. Hii ndiyo Imani Katholiko; * Kila mtu asiyeikubali kwa moyo hawezi kuokoka.
    Atukuzwe.

    Ant. Hii ndiyo Imani Katholiko; Ambayo kwamba kila atakaye kuokoka imempasa kuishika.

Wakati wa Pasaka Ant. hii iachwe, na Imani hii isemwe mara baada ya Zaburi ya mwisho. Ant. ya Zaburi, Haleluya, Ha1eluya,* Haleluya, isemwe hapa mwisho wa Imani.

Imani hiyo isisemwe tangu Alhamisi ya Amri hata S. B. baada ya Pasaka.

Athanasian Creed

 

Return to the Zanzibar Prayer Book

Web author: Charles Wohlers U. S. EnglandScotlandIrelandWalesCanadaWorld