The Book of Common Prayer
United States England Scotland Ireland Wales Canada World

    Chuo cha Sala ya Umoja (1662)
The 1662 Book of Common Prayer in Swahili

 

TARATIBU YA KUWAANGALIA WAGONJWA

Mtu atakapokuwa hawezi, hupewa habari yule Padre wa mipaka ya msikiti ule; naye akiisha kuingia nyumbani kwa yule aliye hawezi, hunena,

AMANI na iwe juu ya nyumba hii na wote wakaao humu.

Akiisha kupata kwa yule aliye hawezi, hupiga magoti na kunena,

USIKUMBUKE makosa yetu, ewe Bwana, wala makosa ya babazetu ; wala usitwae kisasi cha madhambi yetu; utusamehe, Bwana mwema, utusamehe watu wako, uliowakomboa kwa damu yako ya thamani, wala usitukasirikie milele.
    Huitika. Utusamehe, Bwana mwema.

Ndipo hapo yule Padre hunena,

Na tuombe.

Bwana, uturehemu.
    Kristo, uturehemu.
Bwana, uturehemu.
 

Visitation of the Sick

BABAETU uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako na uje, Mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, Kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kututosha. Nawe utusamehe makosa yetu, Kama nasi tulivyowasamehe watukosao. Nawe usitupeleke katika kujaribiwa, Utuokoe maovuni. Amina.

    Padre. Ewe Bwana, umwokoe mtumishi wako,
    Huitika. Akutumainiye.
    Padre. Umletee msaada utoke pahali patakatifu pako;
    Huitika. Umlinde milele kwa uwezo mkuu.
    Padre. Yule adui na asipate nafasi kwake
    Huitika. Wala asimkaribie na kumdhuru yule mtu mwovu.
    Padre. Ewe Bwana, uwe kwake ukuta ulio imara;
    Huitika. Kumkinga na uso wa adui wake.
    Padre. Ewe Bwana, utusikize maombi yetu;
    Huitika. Kilio chetu kikufikilie utiko.

Padre

EWE Bwana, utuangalie huko uliko mbinguni, nawe umtazame huyo mtumishi wako, umwangalie kwa kumsaidia; nawe umwonee huruma, umpe kutua moyo na kutumaini kwako wewe; umkinge na shari la adui, nawe umweke daima katika raha na salama: kwa Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.

UTUSIKIZE, ewe Mungu, Mweza-wa-yote, Mwenye rehema zisizo kifani, Mwokozi wetu, umsongezee wema huyu mtumishi wako kama mazoea yako, ambaye yu katika kusumbuka kwa maradhi. Nawe umtakase kwa hivi umtiavyo adabu kwa mkono wako wa ubaba, ili kwamba kwa hivyo ajionavyo kuwa hana nguvu, aongezeke nguvu katika imani yake, zaidi na toba yake aliyotubu izidi kuwa ya maana; ili kwamba wewe upendapo kumrejeza ile hali ya afya ya siku zote, awe kuyapisha maisha yake yaliyosalia katika kukucha wewe na kukutukuza: au, umpe neema ayakubali hayo uliyompiga, ili kwamba, baada ya kwisha kukoma maisha haya ya mashaka, awe mtu wa kuishi milele pamoja nawe katika maisha yasiyo ukomo; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

Ndipo hapo yule Padre humwonya yule aliye hawezi, kwa kusema kama haya:

EWE mpenzi, neno hili jua sana, ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa maisha na wa kufa, na yaliyohusika nayo yote, nayo ni ujana, nguvu, afya, uzee, unyonge, ugonjwa. Basi maradhi yako yawayo yote, neno hili moja fahamu sana, ya kuwa ni amri ya Mungu. Na sababu yake iwayo yote hata ukapatikana na mateso haya; ikiwa ni kutaka kukujaribu ulivyo na uvumilivu ili kuwaonya wenzio, na kuonekana wazi imani yako uliyo nayo, ionekane katika siku ya Bwana kuwa ni imani ya kusifiwa na kutukuzwa na kuheshimiwa, kwa kuzidi utukufu na hali njema isiyo ukomo; au ikiwa unaletewa kwa kukurudi na kukutia adabu .kwa mambo yako yachukizayo machoni mwake Babaako wa mbinguni: lakini, jua hakika ya kwamba ukitubia kwa madhambi yako toba ya kweli, nawe ukistahimili ugonjwa wako kwa uvumilivu, kwa kutegemea kwa rehema zake Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Yesu Kristo Mwanawe mpenzi wake, na kumshukuru miguuni pake kwa hivyo alivyokurudi kwa mkono wake wa ubaba, kwa kujinyenyekeza kabisa chini ya mapenzi yake: amri hii itageuka iwe faida, nayo itakusongeza mbele katika hiyo njia njema ifikishayo kwenye uzima wa milele.

Na akiwa hawezi sana yule aendewaye, yule Padre na asimsomee zaidi katika maonyo yake; ila yule awezapo, huendelea mbele kunena,

BASI wewe uwe radhi kwa kurudiwa kwako na Bwana, kwani ni kama vile anenavyo mtakatifu Paulo, Waraka wa Wahibirania, Mlango wa kumi na mbili; Huyo ambaye Bwana ampenda humrudi, naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa kwenu mwavumilia; Mwenyezi Mungu awatendea kama wana; kwani ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kwamba hamna kurudiwa, na watu wote wameshiriki kurudiwa, hapo ndipo mmekuwa wana-wa-haramu, si wana-wa-halali. Na hayo yote, tulikuwa ria baba zetu za mwili kuturudi, nasi tuliwastahi: je, hatutajiweka afadhali sana chini yake yeye Baba wa roho zetu, tuwe hai? Kwani wao kweli siku chache waliturudi kama walivyoona vyema wenyewe; ila yeye kwa kutufaa, tupate kutwaa sehemu ya utakatifu wake.
    Maneno haya, ewe ndugu yangu, yameandikwa katika Chuo kitakatifu kwa kutufariji roho zetu na kutufunza, ili kwamba tuvumilie kwa saburi na shukrani turudiwapo na Babaetu wa mbinguni, kila apendapo kwa wema wake wenye neema kuturudi hivyo. Wala halipatikani neno la pili, la kuwafariji Wakristo mioyo yao, kama hilo la kulinganishwa kwao na Kristo, watakaposubirishwa mioyo yao kwa kuvumilia misiba na mashaka na maradhi. Kwani yeye mwenyewe hakupaa juu kwenda furahani kwake, ila alipokwisha kupatikana kwanza na maumivu na mateso; hakuingia utukufuni mwake kabla ya kuteseka kwake msalabani. Nasi hakika yetu ni vivyo; tutesekavyo pamoja na Kristo imekuwa ndiyo njia yetu ya kuingia .katika furaha ya milele; na tufavyo kufa kwa furaha pamoja na Kristo, imekuwa ndio mlango wetu wa kuingia katika maisha ya milele; ili kwamba tuwe watu wa kufufuka kutoka kwa wafu, kwenda kuketi pamoja naye katika maisha yasiyo ukomo. Haya basi, huu ugonjwa wako ulivyo na manufaa kwako, mimi nakusihi uupokee kwa uvumilivu na upole, tena nakunasihi kwa jina lake Mwenyezi Mungu, uyakumbuke uliyoyakiri kwa Mwenyezi Mungu zamani za kubatizwa kwako. Na kwa maana ya tusivyokuwa na budi ya kutozwa hesabu ya maisha haya na yule Mwamuzi wa haki, yule ambaye imepasa watu wote kuamuliwa mbele zake pasipo kuangaliwa uso wa mtu awaye yote; mimi kwa ajili ya hayo nakuambia hivi sasa uangalie nafsi yako na hali yako, ulivyokaa mbele za Mwenyezi Mungu na mbele ya watu; ili kwamba kwa kujishtaki mwenyewe na kujihukumu na kujilaumu kwa makosa uliyoyakosa, upate rehema mikononi mwa Babaetu wa mbinguni kwa ajili yake Kristo, usije ukashtakiwa na kulaumiwa katika hukumu ya siku ile ya utisho. Basi mimi nitakutajia Sharti za Imani yetu, upate kujijua, wayaamini yampasayo mtu wa Kikristo, au huyaamini.

Ndipo hapo yule Padre huzitaja Sharti za Imani kwa kunena;
 

Lord's Prayer

JE, wewe waamini kwa Mwenyezi Mungu Baba, Muumba mbingu na nchi ?
    Na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Mzaliwa pekee, Bwana wetu? Na ya kuwa alitungishwa mimba na Roho Mtakatifu, akazaliwa na Mwanamwali Mariamu; tena kuwa aliteswa katika enzi ya Pontio Pilato; akasalibiwa, akafa, akazikwa; kisha alishuka akaingia kuzimu, hata kwa siku ya tatu akasimama tena, ametoka kwa wafu; kisha alipaa akaingia na mbinguni; tena amekaa upande wa mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu Baba; naye kutoka huko atakuja tena, katika mwisho wa ulimwengu, apate kuwaamua walio hai hata waliokufa?
    Nawe waamini kwa Roho Mtakatifu; Kanisa takatifu lililo ulimwenguni mote; Ushirika wa watakatifu; Madhambi kusamehewa; Mwili kufufuka; na Maisha ya milele baada ya mauti?

Yule aliye hawezi hujibu,

Haya yote ninakubali sana kuyaamini.

Ndipo hapo yule Padre hupeleleza katika kutubia kwake kwa makosa yake, kumwangalia kwamba ametubu kweli, na kwamba yu katika mapendano na watu wote wa ulimwenguni, naye humwonya ya kuwasamehe kwa ndani ya moyo wake watu wote kadiri ya waliomtenda uovu. Na kwamba amemtenda mwenziwe awaye yote uovu, humwonya ya kumtaka msamaha; na kwa kila alilomkosa mtu au kumdhilimu, humwambia amrudishie kila mmoja kadiri ya awezavyo. Na kwamba kabla ya wakati huo hajausia vitu vyake vifanyweje, na aonywe kuandika hati ya kuwarithisha watakaomrithi, na kuyaweka wazi madeni aliyo nayo, awiwayo, au awiayo yeye, ili kuusafi sawasawa moyo wake mwenyewe na kuwastarehesha mawasii watakaogawanya mali yake yatakayorithishwa. Nao imewapasa watu kukumbushwa mara kwa mara ya kuusia vitu vyao vya duniani kwa kutengeza urithi wake wakali na afya na uzima.

Maneno hayo yaliyokwisha kutajwa, husemeka kwanza asijasali yule Padre, kama aonavyo kupasa.

Yule Padre na asiache kuwaonya sana wagonjwa hao awaonao kuwa waweza, ili wapate kuwapa maskini kwa ukarimu.

Wakati huu yule mgonjwa huonywa ya kuungama madhambi yake, kwamba ajiona amelemewa moyo wake na neno lililo zito kwake lolote, naye baada ya kule kuungama hupewa msamaha na yule Padre (akiwa yuataka kama hayo kwa kupenda na kunyenyekea) kwa kunena kama haya,

BWANA wetu Yesu Kristo, aliyeliachia kanisa lake amri kuwapa msamaha wa madhambi yao wenye dhambi wote watubuo kweli, na kuamini kwake, kwa rehema zake zilizo kuu na akusamehe makosa yako. Nami kwa amri yake niliyowekewa, juu yangu, nakupa msamaha wa madhambi yako yote, kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.

Ndipo hapo yule Padre huisoma sala hii;

Na tuombe.

EWE Mwenyezi Mungu, rehema zako ni nyingi sana, nawe kwa wingi wa hizo rehema wawaondolea ma dhambi yao hao watubuo kweli, hata umekuwa huyakumbuki kamwe; umwangalie kwa huruma huyu mtumishi wako, atakaye sasa msamaha na ondoleo la madhambi. Nawe Baba uliye mwingi wa kupenda, mrejezee upya yaliyoharibika ndani yake, kwa udanganyifu na uovu wa Shetani, au kwa mapenzi yake ya mwilini na ule unyonge wake alio nao; kia hiki kilicho hakiwezi ukiponye nawe ukidumishe katika umoja wa kanisa; umwangalie alivyopondeka moyo, umkubalie machozi yake, umpunguze maumivu yake, kwa hivyo utakavyoona ni vya kumfaa. Nawe kwa maana ya alivyozitumainia rehema zako, hizo tu, usimhesabie makosa yake ya tangu hapo, bali umtie nguvu kwa Roho wako Mwenye-baraka; hata utakapopenda kumwondoa huku, uwe kumchukua hata kwenye radhi yako, kwa alivyostahili Mwanayo umpendaye sana, Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.

Ndipo hapo yule Padre husoma Zaburi hii:

In te, Domine, speravi.   Zaburi 71

NIMEKUKIMBILIA wewe, ewe Yehova: nisiaibike milele.
  2. Kwa haki yako uniponye, uniopoe: unitegee sikio lako, uniokoe.
    3. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu nitakakokwenda siku zote; umeamuru niokolewe; ndiwe genge langu na ngome yangu.
    4. Ewe Mungu wangu uniopoe katika mkono wa mtu asiye haki : katika mkono wa mtu mwovu, dhalimu.
    5. Kwani ndiwe taraja langu, ewe Bwana Yehova : tumaini langu tokea ujana wangu.
    6. Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa, ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu : nitakusifu wewe daima.
    7. Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi : na wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.
    8. Kinywa changu kitajazwa kwa sifa zako : na kwa heshima yako mchana kuchwa.
    9. Usinitupe wakati wa uzee : nguvu zangu zipungukapo usiniache.
    10. Kwa maana adui zangu wananiamba : na wanaoniotea nafsi yangu hufanya shauri pamoja.
    11. Wakisema, Mungu amemwacha : mfuatieni mkamateni, hakuna wa kumponya.
    12. Ewe Mungu, usiwe mbali nami : ewe Mungu wangu, ufanye haraka kunisaidia.
    13. Waaibishwe, watoweshwe adui za nafsi yangu : wavikwe laumu na fedheha wanaonitakia mabaya.
    14. Nami nitatumaini daima : nitazidi kuongeza sifa zako zote.
    15. Kinywa changu kitasimulia haki yako : na wokofu wako mchana kuchwa, kwani sijui hesabu yake.
    16. Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Yehova : nitataja haki yako wewe peke yako.
    17. Ewe Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu : nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata hivi leo.
    18. Na hata sasa nikiwa mzee mwenye mvi, usiniache, ewe Mungu : hata niishe kuwaeleza watu wa kizazi hiki nguvu zako; na kila atakayekuja uwezo wako.
    19. Na haki yako, ewe Mungu, imefika juu sana : wewe uliyefanya mambo makuu; ewe Mungu, ni nani aliye kama wewe?
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu ;
    Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Na huku aongeza maneno haya,

EWE Mwokozi wa ulimwengu, wewe ambaye kwa Msalaba wako na Damu yako ya thamani ulitukomboa, utuokoe utuletee msaada, twakuomba miguuni pako, ewe Bwana.

Ndipo hapo hunena yule Padre,

BWANA, ambaye ndiye Mweza-wa-yote naye ni ngome iliyo imara sana kwa wote hao wamtumainio, naye kwake vitu vyote vya mbinguni na vya duniani na vya chini ya dunia humsujudia na kumtii; basi Bwana huyo na awe ulinzi wako wewe, hivi sasa na milele, na akupe kujua na kufahamu neno hili, ya kwamba hakuna tena jina jingine chini ya mbingu, walilopewa wanadamu, ambalo mumo wapata kupokea afya na wokofu, ila jina lake Bwana wetu, Yesu Kristo, hilo tu. Amina.

Kisha baadaye hunena,

TWAKUTIA katika rehema na ulinzi alizotufadhili Mwenyezi Mungu: Bwana na akubarikie akulinde. Bwana na akukunjulie uso wake akuneemeshe: Bwana na akuinulie uso wake akupe na salama, sasa, na milele. Amina.
 

Articles of Faith

Sala ya kumwombea mtoto aliye hawezi

EWE Mungu Mweza-wa-yote, Baba mwenye rehema, kwamba ni kuishi kwamba ni kufa pia yana wewe pekeo; sisi tu miguuni pako twakuomba huko uliko mbinguni umwangalie kwa rehema mtoto huyu, amelala hapa kitandani ali hali ni mgonjwa: umwangalie kwa wokofu wako, Bwana; nawe kwa majira uyaonayo yatafaa umponye na maumivu yake ya mwilini, uiokoe roho yake kwa ajili ya rehema zako: ili kwamba (utakapopenda kuzifanya nyingi siku zake za humu ulimwenguni) aishi katika kukulekea wewe, kisha awe chombo cha kuonyesha utukufu wako, kwa kukutumikia kwa uaminifu na kufanya ambayo yatavutia faida zamani zake. Au, umkaribishe katika hayo maskani ya mbinguni zikaamo roho zao waliolala katika Bwana Yesu, hali ya raha na furaha za milele. Nawe utupe haya, Bwana, kwa ajili ya rehema zako, kwa yeye Mwanayo Bwana wetu, Yesu Kristo, aishiye na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja, milele. Amina.
 

Prayer for a Sick Child

Sala ya kumwombea aliye hawezi, amwonapo kwamba hatapoa

EWE Baba wa rehema, Mungu wa utulizi wote, Msaada wetu kila wakati wa dhiki ni wewe pekeo; tumekukimbilia wewe kwa kukuomba kwa ajili ya huyu mtumishi wako, ali hali amelala hapa chini ya mkono wako na unyonge mwingi wa mwilini. Umtulizie macho yako ya rehema, ewe Bwana: na kama utakavyoharibika mwili, nawe uzidi kumpa nguvu, kwa neema yako na Roho wako Mtakatifu, katika nafsi yake ya ndani. Nawe umpe kutubia toba isiyo shaka ya makosa yote ya maisha yake yaliyopita, na imani iliyokaza katika Mwanayo Yesu; ili kwamba dhambi zake ziondolewe kwa rehema yako, naye apigiwe muhuri wa msamaha wake mbinguni, kabla asijaondoka huku akawa kutoonekana tena kwetu. Tumejua, Bwana, ya kwamba hakuna neno kwako wewe lisilowezekana, na ya kuwa hata hivi waweza kumwinua ukamrejeza afya, ukiwa wapenda, apate kwendelea katika kukaa mwetu; ila, pamoja na haya, kwa maana ya kuwa aonekana kuwa amekaribia kuingia katika kufariki, twataka kwako ya kumtengeza na kumweka tayari kwa saa ya kufa, hata iwe, baada ya kuondoka kwake huku na amani yako na neema, kuwa roho yake yakaribishwa katika ufalme wako usio mwisho; kwa kustahili kwake na uombezi wake Mwanayo pekee, Bwana wetu, Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Amina.
 

Pryaer for a sick Person when there is little hope for Recovery

SALA ya kuiombea roho ya mtu aliye hawezi, katika muda wa kufariki kwake

EWE Mungu, Mweza-wa-yote, zaishi kwako wewe roho za wenye haki waliokamilika baada ya kwisha kufunguka hivyo vifungo vyao vya duniani: basi sisi tulio hapa miguuni pako twaitia roho yake huyu ndugu yetu tumpendaye katika mikono yako wewe, nayo ndiyo mikono ya Muumba aliye mwaminifu, mikono ya Mwokozi aliye mwingi wa rehema; na huku twataka kwako iwe ya thamani machoni mwako roho hii. Twakuomba uioshe katika damu ya yule Mwana-wa-kondoo asiye kosa, aliyechinjwa kwa kuondoa dhambi za ulimwengu, ili kwamba yangawaje hayo mambo ya unajisi yaliyoipata ili humu katika ulimwengu huu dhaifu na upotofu, kwa tamaa za mwili au udanganyifu wa Shetani, lakini (kwa kutakaswa na kuondolewa hizo zote) iwe kuletwa mbele zako wewe hali ya kutakata pasipo kipaku kiwacho chote. Na sisi tuliosalia hali tuli mumu katika mambo haya ya mauti yaliyo machoni mwetu kila siku, utufunze kujijua hali yetu wenyewe tulivyo wanyonge, na tulivyo watu tusiojua siku zetu zilivyo, utufunze na kuzihesabu siku zetu sana, hata tuwe kuitia mioyo yetu katika hekimahiyo takatifu ya mbinguni, siku zote tuishizo hapa; nayo hekima hiyo ndiyo itakayotusongeza hatima yake katika maisha yasiyo mwisho; kwa fadhili zake na kustahili kwake Mwanayo pekee, Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.
 

Commendatory Prayer for a sick Person at the point of Departure

Sala ya kuwaombea hao wasumbukao katika mioyo yao au dhamiri zao

EWE Bwana Mwenye-baraka, wewe ndiwe Baba wa kila rehema, nawe u Mungu wa utulizi wote; twataka kwako umwangalie kwa huruma na rehema huyu mtumishi wako atesekaye. Wewe umemwandikia machungu, nawe u katika kumkumbusha viovu vyake vya tangu hapo: ghadhabu zako zimekaza kumlemea; nafsi yake nayo imejaa huzuni; lakini wewe, ewe Mungu mwenye rehema, uliyeandika Neno lako kwa ajili ya kutufunza sisi, ili kwamba kwa vile tutakavyopata uvumilivu na utulivu mumo katika Maandiko yako matakatifu, tupate taraji na matumaini; umpe mtu huyu fahamu za kuijua nafsi yake sawasawa, tena kuufahamu sawasawa utisho wako na ahadi zako; asije akatupa tumaini lake alilo nalo kwako, wala asiliweke pahali pengine isipokuwa kwako wewe. Umpe nguvu za kujizuia na majaribu ajaribiwayo yote, nawe umpoze magonjwa yake yote. Huu mwanzi uliopondeka usiuvunje, hii katani ifukayo moshi usiizime. Wala usizuie huruma zako za ndani kwa kasirani; bali msikizishe mtu huyu ya furaha na nderemo, ili kwamba mifupa uliyoivunja ipate kufurahi. Umwokoe na utisho wa adui, umwinulie na mwanga wa uso wako, umpe raha na amani, kwa kustahili kwake na uombezi wake Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.
 


 

Prayer for Persons troubled in Mind or Conscience

WALIO HAWAWEZI KUWASONGEZEA USHIRIKA

Kwa maana ya kuwamo wanadamu wote katika hatari aina nyingi, na magonjwa na maradhi mengine mengine ya ghafula, na kule kukaa kwao kila mmojawapo hali hajui wakati wake atakaofariki dunia; kwa ajili ya hayo, ili kwamba kuwaacha wakakaa tayari daima, wali hali ipasayo katika kufariki, pindi Mwenyezi Mungu atakapoona vyema kuwaita, wale Mapadre na wafanye bidii mara kwa mara kuwaonya walio mipakani mwa kila msikiti, kwamba wawe katika kuupokea mara kwa mara Ushirika Mtakatifu wa Mwili na Damu vyake Mwokozi wetu Kristo, utahaposongezwa mbele ya watu msikitini; ili wafanyapo kama hayo, wakikutwa na neno la ghafula wapungue kusumbuka, uwapo Ushirika huo haupatikani. Lakini akiwa yule mgonjwa hawezi kwenda msikitini, naye yuataka kuupokea Ushirika kwake nyumbani; ndipo hapo yule mgonjwa humpa habari yule Padre na mapema, na kumjuvya hesabu ya hao ambao watashirikiana pamoja naye, ni watu wangapi (nao hawapungui watu watatu hesabu yao, au uchache ni wawili) ; na akipata pahali nyumbani mwake yule aliye hawezi, ambapo hufaa kwa haja ile, pamoja na vitu vyote vitakwavyo, vimetengea sawasawa, hata apate yule Padre kuusongeza kwa heshima ule Ushirika; basi pahali hapo yeye huufanya Ushirika Mtakatifu, kwa kusoma mbele Sala hii na Waraka huu na Injili hii:
 

Communion of the Sick

Sala

EWE Mungu, Mweza-wa-yote, Mkazi wa milele, Muumba wa binadamu, ndiwe mwenye kuwarudi uwapendao, na kumtia adabu kila mtu umkubaliye; twa omba sana umrehemu huyu mtumishi wako, uliyemrudi kwa mkono wako, umpe kustahimili huu ugonjwa wake kwa uvumilivu, arejee afya yake ya mwilini, kwamba ndiyo mapenzi yako ya neema, naye atakapokuwa mwili kutokwa na roho yake, iwe hiyo kusongezwa pasipo kosa kwako wewe: kwa Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.
 

Collect

Waraka. Wahibirania 12. 5-6

MWANANGU, usione kuwa ni kudogo kurudiwa kwa Bwana, wala usizime moyo ukikaripiwa naye; kwani huyo ambaye Bwana ampenda humrudi, naye humpiga kila mwana amkubaliye.
 

 

Injili. Yohana 5. 24

NI kweli, ni kweli, nawaambia ya kwamba, mwenye kusikia neno langu, na kumwamini aliyenileta, yuna uzima wa milele, wala haingii katika hukumu, ila amekwisha kupita kutoka mautini kuingia uzimani.

Kisha baadaye yule Kasisi huendelea kusoma kwa kuifuata kawaida iliyokwisha kuagizwa ya Ushirika Mtakatifu, naye huanza penye maneno haya, Ninyi mtubiao kwa dhambi zenu kwa kweli (w.k.).

Hata muda wa kuugawanya ule Ushirika Mtakatifu, yule Kasisi huanza kwa kuupokea Ushirika Mtakatifu nafsi yake, kisha baadaye huwasongezea wao waliowekwa kuwa watu wa kushirikiana na aliye hawezi; hatima yake humsongezea yule mtu aliye hawezi.

Lakini akipatikana mtu, ambaye kwa ulivyokwenda mno ule ugonjwa wake, au kwa kukosekana neno lolote, kwamba ni kutomwambia mbele sawasawa yule Kasisi, kwamba ni kutopata kikao cha watu ambao watashirikiana naye, kwamba ni kizuizi cha haki kingine kiwacho chote, haupokei Ushirika wa Mwili na Damu vyake Kristo; hapo ndipo yule Kasisi humweleza ya kwamba atubiapo kweli yale madhambi yake, na kukaza kuamini ya kuwa Yesu Kristo amepatikana na mauti juu ya msalaba kwa ajili yake, hata ametokwa na damu yake nayo kwa kumkomboa, naye ayakumbukapa kwa bidii manufaa aliyoyapata katika hayo, akawa na kumshukuru shukrani za moyoni kwa ajili ya hayo; mambo haya ayafanyapo yule mgonjwa, na ajue kuwa huku ndiko kula na kunywa Mwili na Damu vyake Mwokozi wetu kwa kufaa, nako huivutia afya roho yake, na angawa haupokei ule Ushirika midomoni mwake.

Na yule mgonjwa akiangaliwa, naye wakati uo huo akaupokea Ushirika Mtakatifu, ndipo hapo yule Kasisi, kwa ajili ya kufupiza mambo kwa kuyaendeleza kwa upesi zaidi, huimaliza ile kawaida kabla asijaisoma Zaburi ya Nimekukimbilia wewe, ewe Yehova, na kwendelea mara kuusoma Ushirika.

Na zamani za tauni au maradhi, au zamani nyingine kama hizo, za wito wa maradhini au magonjwani, pasipopatikana miongoni mwa watu wa mipaka ya msikiti mle wala jirani, watu ambao wataka kushirikanishwa na walio hawawezi nyumbani mwao, kwa ajili ya kuchelea kupatikana na wito, atakwapo yule Kasisi na yule mwenye maradhi hayo, huweza kushirikiana naye yeye pekee.

 

 

Return to the 1662 Book of Common Prayer in Swahili

Web author: Charles Wohlers U. S. EnglandScotlandIrelandWalesCanadaWorld