The Book of Common Prayer
United States England Scotland Ireland Wales Canada World

    Chuo cha Sala ya Umoja (1662)
The 1662 Book of Common Prayer in Swahili

 

ZABURI ZILIZOKHUSIKA NA SIKU KUU
 
 
Asubuhi
Jioni
Siku ya Uzazi wa Bwana
Zaburi 19
45
85
Zaburi 89
110
132
Jumatano ya Ivu
Zaburi 6
32
38
Zaburi 102
130
143
Juma Njema
Zaburi 22
40
54
Zaburi 69
88
Siku ya Kufufuka kwa Bwana
Zaburi 2
57
111
Zaburi 113
114
118
Siku ya Kupaa
Zaburi 8
15
21
Zaburi 24
47
108
Pentecost
Zaburi 48
68
Zaburi 104
145

 

 

Psalms for Holy Days

TARATIBU YA SALA YA ASUBUHI YA KILA SIKU MWAKA MZIMA

Mwanzo wa Sala ya Asubuhi yule Padre husoma kwa sauti kuu aya moja au zaidi ya Maandiko Matakatifu katika hizo zilizowekwa : kisha hunena yafuatanayo na aya hizo.

MTU mbaya atakapotubu na kuuacha huo ubaya wake alioufanya, akayafanya yaliyo halali na haki, ataiponya nafsi yake awe hai.   Ezekieli 18. 27
    Ninakiri mimi makosa yangu, na dhambi yangu i mbele yangu daima.   Zaburi 51. 3
    Ufiche uso wako, usitazame dhambi zangu, uzifute hatia zangu zote.   Zaburi 51. 9
    Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika: moyo uliovunjika na kupondeka, ewe Mungu, hutaudharau.   Zaburi 51. 17
    Rarueni mioyo yenu, msirarue mavao yenu, nanyi rejeeni kwa Yehova Mungu wenu: kwa kuwa yeye ni mwenye neema na huruma: si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema: naye hujutia lile shari.   Yoeli 2. 13
    Ni ya Yehova Mungu wetu huruma na msamaha, kwani mmemwasi, wala hatukusikiza sauti ya Yehova Mungu wetu kwa kwenenda katika sheria yake aliyotuwekea mbele yetu.   Danieli 9. 9-10
    Ewe Yehova, nirudi, ila kwa haki, si kwa hasira, usije ukanidhili.   Yeremia 10. 24
    Tubuni, kwani ufalme wa mbingu umekwisha kukaribia.   Mathayo 3. 2
    Nitaondoka, niende kwa baba, nikamwambie, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele zako; sistahili tena kuitwa mwanayo.   Luka 15. 18-19
    Ewe Yehova, usimhukumu mtumishi wako; kwani mbele zako hakuna aliye hai atakayehesabiwa kuwa ni mwenye haki.   Zaburi 143. 2
    Ikiwa twanena ya kwamba hatuna dhambi, twapoteza nafsi zetu, na hiyo kweli haimo ndani yetu. Ila ikiwa twaziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu kisha yuna haki akatusamehe dhambi zetu na kutusafi na uovu wote.   1 Yohana 1. 8-9
 

Morning Prayer

Ni roho Mwenyezi Mungu; nao wenye kumwabudu imewapasa kuabudu katika roho na kweli.   Yohana 4. 24
    Mwabuduni Yehova kwa uzuri wa utakatifu; tetemekeni mbele zake, nchi yote.   Zaburi 96. 9
    Usiku umekwendelea sana, mchana umekaribia: basi na tuzivulie mbali zile kazi za giza, na kujivisha silaha za mwanga.   Warumi 13. 12

Uzazi wa Bwana wetu, au Christmas
    Ninawahubirini habari nzuri za furaha nyingi zitakazokuwa ni za wenyeji wote; kwani leo amezaliwa kwa ajili yenu katika mji wa Daudi, Mwokozi, naye ni Kristo Bwana.   Luka 2. 10-11
    Katika neno hili hayo mapenzi ya Mwenyezi Mungu yamefanywa wazi ndani yetu sisi, ya kwamba Mwenyezi Mungu amemtuma Mwanawe mzaliwa pekee aingie duniani, ili kwamba tupate kuwa hai kwa yeye.   1 Yohana 4. 9

Mafunuo
    Tokea kucha kwake jua hata kutua kwake lilo, jina langu ni kuu katika watu wa hao mataifa; tena kila pahali uvumba wasongezwa katika jina langu, na dhabihu iliyo safi: kwa kuwa jina langu ni kuu katika watu wa hao mataifa, asema Yehova wa majeshi.   Malaki 1. 11
    Yehova ameujulisha wokofu wake; machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake.  Zaburi 98.2

Mateso
    Angalieni, mwone kwamba pana majonzi mengine yawayo yote yaliyo mfano wa majonzi niliyo nayo mimi, hayo niliyotendewa.   Maomboleo 1. 12

Ijumaa Njema
    Mwenyezi Mungu ayadhihirisha kwetu mapenzi yake mwenyewe aliyetupenda, kwa maana, tulipokuwa tukali wenye dhambi, Kristo akafa kwa ajili yetu.   Warumi 5. 8
    Siku iliyo kabla ya Ufufuo Ukae kimya mbele za Yehova, ukamngojee wala usikasirike; naye atakupa haja za moyo wako.   Zaburi 37. 7,4

Ufufuo
    Na ashukuriwe Mwenyezi Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye katika rehema zake kuu, ametuzaa sisi mara ya pili kwa njia ya kufufuliwa kwake Yesu Kristo.   1 Petero 1. 3

Siku ya Kupaa
    Kwa kuwa tuna kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu Mwana wa Mwenyezi Mungu, na tukiendee hicho kiti-cha-neema kwa uthubutifu, ili kwamba tupate rehema na kuona neema-ya kutusaidia wakati wa haja.   Wahibirania 4.14, 16

Pentecost
    Mapenzi ya Mwenyezi Mungu yamekwisha kumiminwa na kutiwa. ndani ya mioyo, yetu na Roho Mtakatifu ambaye tumepewa sisi.   Warumi 5. 5

Utatu
    Mwenyezi Mungu ni mapenzi; na yeye akaaye katika mapenzi yuakaa ndani ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu yuakaa ndani yake yeye.   1 Yohana 4. 16

Watakatifu Wote
    Kwa kuwa tumezingirwa na wingu kubwa la mashahidi jinsi hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na hiyo dhambi iliyotuzunguka sisi kwa wepesi, na tupige mbio kwa uvumilivu kwa yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanziliza na mwenye kutimiliza imani yetu.   Wahibirania 12. 1-2

Siku za Watakatifu
    Mwenye haki atakumbukwa milele. Kuwakumbuka hao wenye haki huwa na baraka.   Zaburi 112. 6; Mifano 10. 7

Mwaka Mpya
    Hao wamngojeao Yehova watarejeza upya nguvu zao; watakwea juu kwa mabawa mfano wa kipungu ; watapiga mbio, wasichoke; watakwenda kwa miguu, nao hawatazima roho.   Isaya 40, 31

Mavuno
    Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Yehova.   Zaburi 24.1

Wakati wa Mashaka
    Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu: msaada uonekanao wakati wa mateso.    Zaburi 46. 1

Mambo ya Ufalme
    Mataifa wafurahi na kuimba kwa furaha: kwani wewe utawahukumu watu kwa haki, utawaongoza watu walioko duniani.   Zaburi 67. 4

The following introductory sentences are additions, and are optional.
 
ENYI ndugu zangu mpendwao sana, twaonyeshwa katika Maandiko mwahali kadhawakadha, ya kukiri na kuyaungama madhambi yetu na viovu vyetu kila namna; pasipo kuvificha wala kuvifinika mbele ya uso wa Mwenyezi Mungu Babaetu wa mbinguni: twaonyeshwa ya kuviungama kwa moyo wa unyonge na unyenyekevu, wenye kutubia na kufuata; ili kwamba kwa wema wake na rehema zake zisizo ukomo, tupate kusamehewa. Nasi ingawa kule kumwekea wazi Mwenyezi Mungu madhambi yetu kwa uynyenyekevu ni neno litupasalo sana kila wakati; ni zaidi sana wakati tukutanapo wenyewe kwa wenyewe, kuja kumshukuru kwa rehema kuu tulizopokea mikononi mwake, na kumsifu kama ilivyopasa sana, na kusikiza Neno lake lililo takatifu, na kumtaka kadiri ya tulivyo na haja navyo, rohoni hata mwilini. Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nawasihi ninyi nyote mliopo, mfuatane nami kwa mioyo myeupe, na sauti nyenyekevu, tuje tukaribie katika kiti cha neema ya mbinguni, mseme nyuma yangu;
 
Invitation to Confession

Hapa Padre aweza kusema maneno kama haya, akiona ni vizuri;

TUKIWA tumepiga magoti, na tukae kimya kwa dakika chache, tukikumbuka ya kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi hapa.
 

A shorter, optional invitation to Confession

Haya ni maneno ya watu pia wote, ya kuungama makosa, nayo husemwa na watu wote nyuma yake yule Padre, hali wamepiga magoti pia wote.

EWE Baba, Mwenyezi, Mwingi wa rehema; Sisi tumekosa, Tumepotea njia zako, kama kondoo waliopotea Tumefuata mno mashauri na tamaa za mioyo yetu wenyewe. Tumekosa sheria zako takatifu. Yaliyopasa kuyafanya hatukuyafanya, Tumefanya yasiyotupasa kuyafanya: Wala hatuna salama ndani yetu wenyewe. Ila wewe, Bwana, uturehemu, sisi wakosaji dhaifu: Ewe Mungu, uwasamehe wenye kuyaungama makosa yao. Uwakubali waliotubia : Kama ahadi zako walizofunuliwa wanadamu katika Kristo Yesu, Bwana wetu. Kisha, Baba mwingi wa rehema, Utupe kwa ajili yake yeye; Ya sisi kuishi tangu leo maisha ya uchaji-wa-Mungu na haki na mambo ya kiasi, Kwa kulitukuza jina lako lililo safi. Amina.

Ghofira, au Ondoleo la madhambi: nalo hutamkwa na Kasisi pekee, hali amesimama, watu wakali wamepiga magoti.

MWENYEZI Mungu, Babaye Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye hataki mauti ya mwenye dhambi, afadhali ataka aua che uovu wake awe hai: naye amewapa amri watumishi wake, amewaagiza, ya kuwaeleza na kuwaambia watu wake waliotubia, ya wao kusamehewa na kuondolewa madhambi yao: yeye huwasamehe na kuwaondolea madhambi wote waliotubu kweli, walioamini Injili yake takatifu pasipo kuitilia shaka. Kwa ajili ya hayo na, tumwombe atupe toba ya kweli, atupe na Roho wake Mtakatifu, ili tuyafanyayo hivi sasa yampendeze; na maisha yetu ya tangu sasa yawe safi na utakatifu, ili mwisho tufikilie katika furaha zake za milele; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu.

Hapa na kila pakomapo Sala watu huitika, Amina.

Kisha Padre hupiga magoti na kuisoma Sala ya Bwana kwa sauti ya kusikilikana : na watu nao hali wamepiga magoti, husoma pamoja naye: kwa wakati huo, na kila itumiwapo katika Ibada ya Mwenyezi Mungu.
 

 

 

Confession & Absolution

BABAETU uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako na uje. Mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, Kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kututosha, Nawe utusamehe makosa yetu, Kama nasi tulivyowasamehe watukosao. Nawe usitupeleke katika kujaribiwa; Utuokoe maovuni: Kwa kuwa ufalme, na nguvu, na utukufu, ni vyako milele. Amina.

¶ Kisha husoma,

          Ewe Bwana, ufunue midomo yetu.
Huitika. Na vinywa vyetu vitatangaza utukufu wako.
Padre. Ewe Mungu, utuokoe upesi.
Huitika. Ewe Bwana, utusaidie haraka.

Wakati huo watu wakiisha kusimama wote, Padre husoma,

    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu;
    Huitika. Kama vile mwanzo, na sasa: hata milele ni vivyo. Amina.
    Padre. Msifuni Bwana.
    Huitika. Jina la Bwana lisifiwe.

Hapa husomwa au kuimbwa Zaburi hii ifuatanayo : isipokuwa Idi ya Ufufuo, ndipo Wimbo mwingine uamriwapo : tena na kila siku ya mwezi kumi na kenda haisomwi hapa, ila husomwa. katika taratibu ya Zaburi kama desturi.
 

Lord's Prayer

VENITE EXULTEMUS DOMINO

Zaburi 95

HAYA! na tumwimbie Yehova kwa furaha : na tumo shangilie Mwamba wa Wokofu wetu.
    Twendeni haraka, tukasimame mbele ya uso wake na shukrani : tumshangilie kwa zaburi.
    Kwani Yehova ni Mungu Mkuu : ni Mfalme mkuu, juu ya miungu yote.
    Ambaye mabopo makuu ya dunia ya mkononi mwake : na vilele vya milima pia ni vyake.
    Ambaye bahari ni yake, Mwenyewe aliifanya : mikono yake iliiumba nchi kavu.
    Njoni tukaabudu, tusujudu : tupige na magoti mbele za Yehova mwenye kutufanya.
    Kwani ndiye Mungu wetu : nasi tu watu wa uchunga wake, tu kondoo za mkono wake.
    Leo, lau kwamba mwaisikia sauti yake, msiifanye mizito mioyo yenu : kama mlivyofanya huko Meriba, kama siku ya Masa, mle barani.
    Babazenu waliponionja : walinihakikisha, waliniona nifanyavyo.
    Miaka arobaini nilichukizwa na kizazi kile, nikasema : Wao ni taifa la watu watangao mioyo yao, wala hawakuelewa na njia zangu.
    Ndipo nilipoapa kwa hasira zangu : Hawaingii katika starehe yangu.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana : na kwa Roho Mtakatifu:
    Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Ndipo hapo huandama Zaburi, kwa taratibu yake, kama ilivyoagizwa. Hata baada ya mwisho wa kila Zaburi mwaka mzima, na mwisho wa Benedicite, na Benedictus, na Magnificat, na Nunc Dimittis, husomwa maneno haya,

    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu :
    Huitika. Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Ndipo husomwa wazi kwa sauti ya kusikilikana Somo la Kwanza, katika Agano la Kale, kama ilivyoagizwa katika Kalendari, isipokuwa ni siku iliyoagiiwa Masomo ya kuhusika. Naye mwenye kusoma husimama akajilekeza kwa kuangalia watu wapate kumsikia sana, kadiri ya waliopo. Kisha baadaye na usomwe, au uimbwe, utungo uitwao Te Deum Laudamus kila siku ya mwaka mzima.

Tunza: Ya kwamba mwanzo wa kila Somo, yule mwenye kusoma husema, Mwanzo wa mlango kadhawakadha, wa Chuo kadhawakadha, au Mwanzo wa Kifungu kadhawakadha : Na mwisho wa kila Somo, husema, Somo la Kwanza, au la Pili, limekoma hapo.

TE DEUM LAUDAMUS

TWAKUSIFU Mungu : twakukiri wewe ndiwe Bwana.
    Dunia nzima yakuabudu : Baba uliyeko milele.
    Malaika wote wakupazia sauti : mbingu na nguvu zilizomo zote.
    Makeruhi na Maserafi daima : wakupazia sauti wewe.
    Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu : Yehova Mungu wa majeshi.
    Mbingu na nchi zimejaa : enzi ya utukufu wako tele.
    Wakusifu wewe : jamaa tukufu ya Mitume.
    Wakusifu wewe : kikao chenye sifa njema cha manabii.
    Wakusifu wewe : jeshi safi la mashahidi.
    Kanisa takatifu, duniani mote : lakukiri wewe.
    Baba mwenye enz : isiyo ukomo.
    Mwanayo wa kuheshimiwa : aliye kweli, aliye pekee :
    Tena Roho : Mtakatifu, Msaada.
    Wewe ndiwe Mfalme wa Utukufu : ewe Kristo.
    Wewe ndiwe Mwana wa Milele : wa Baba.
    Wewe, ulipojitia katika kukomboa binadamu : hukuchukizwa na tumbo la Mwanamwali.
    Wewe, uliposhinda uchungu wa mauti : uliwafunulia Ufalme wa mbingu wenye imani.
    Wewe wakaa upande wa mkono wa kuume wa Mungu : enzini mwake Baba.
    Twasadiki ya kwamba utakuja : kuwa Mwamuzi wetu.
    Basi twakutaka wewe, uwasaidie watumwa wako : uliowakomboa kwa damu yako ya thamani.
    Uwape kuhesabiwa katika utukufu wa milele : pamoja na watakatifu wako.
    Uwaweke salama watu wako, Bwana : uubarikie urithi wako.
    Nawe uwatawale : uwainue wao milele.
    Siku hata siku : twakutukuza wewe;
    Na jina lako twalisifu : milele na milele.
    Uwe radhi Bwana : hii siku ya leo utulinde na dhambi.
    Uturehemu Bwana : uturehemu sisi.
    Rehema zako, Bwana, zishuke juu yetu : kama vile tulivyokutumaini wewe.
    Nimekutumaini wewe, Bwana : sitafedheheka milele.
 

Psalm 95

Au utungo huu,

BENEDICITE, OMNIA OPERA

ENYI Kazi zote za Yehova, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Malaika za Yehova, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Mbingu, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Maji yaliyo juu ya Anga, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Nguvu zote za Yehova, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Jua na Mwezi, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Nyota za Mbinguni, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
  Enyi Manyonyota na Umande, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Pepo za Mwenyezi Mungu, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Moto na Chaka, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Masika na Kaskazi, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Umande na Kipupwe, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Maji ya Kuganda na Baridi, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Barafu na Theluji, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Masiku na Michana, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Mwanga na Giza, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Umeme na Mawingu, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Na Nchi nayo imshukuru Yehova : na imsifu, imtukuze milele.
    Enyi Milima na Vilima, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Majani Mabichi yaliyo juu ya Nchi nyote, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Vijito vya Maji, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Bahari, nanyi Mito ya Maji, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Nyangumi, nanyi mtukutao Majini, nyote, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Nyuni za Angani nyote, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi nyote Nyama za Mwitu na za Miji, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Wanadamu, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Isiraeli naye na amshukuru Yehova : amsifu, amtukuze milele.
    Enyi Makuhani wa Yehova, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Watumishi wa Yehova, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Nafsi na Roho za Wenye-Haki, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Watu Watakatifu, Wanyenyekevu wa Mioyo, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Enyi Anania, na Azaria, na Misaeli, mshukuruni Yehova : msifuni, mtukuzeni milele.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu:
    Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Hapo husomwa vivyo Somo la Pili, katika Agano Jipya. Na baadaye Wimbo huu unaoandama, isipokuwa utukiapo huu kusomwa katika Mlango uliohusika na siku yake au ukasomwa kuwa Injili siku ya Mbatizaji Yohana.

BENEDICTUS

Luka 1. 68-79

ASHUKURIWE Bwana, Mungu wa Isiraeli : kwa kuwa amewaangalia watu wake, amewafanyia na ukombozi;
    Tena ametuinulia pembe ya wokofu : katika nyumba ya Daudi mtumishi wake;
    Kama alivyosema kwa vinywa vya manabii wake watakatifu : waliokuwako tangu milele;
    Maana, wokofu katika adui zetu : na katika mikono ya wote watuchukiao;
    Kuwaonea huruma baba zetu : na kukumbuka maagano yake matakatifu;
    Kiapo alichomwapia : babaetu Iburahimu;
    Ya kwamba atatupa : tuli hali tumeokoka na mikono ya adui zetu;
    Kumtumikia pasipo hofu kwa utakatifu na haki : mbele zake siku zetu zote.
    Nawe, kijana wewe, utaitwa Nabii wa Aliye-juu-sana : kwani utamtangulia Bwana mbele ya uso wake, kumtengezea njia zake.
    Ili kuwapa watu wake kuujua wokofu : kwa kusamehewa dhambi zao,
    Kwa huruma za ndani za Mungu wetu : kwa hizo itatuangalia Alfajiri itokayo juu.
    Iwang'arie waketio katika giza na kivuli cha mauti : ili kutuongoza miguu yetu njia ya amani.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana : na kwa Roho Mtakatifu:
    Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Au Wimbo huu katika Zaburi,
 

 

JUBILATE DEO

Zaburi 100

MSHANGILIENI Yehova, dunia nzima : mtumikieni Yehova kwa furaha, njoni mbele zake kwa kutekerea.
    Mjueni Yehova ndiye Mungu : ndiye aliyetufanya, nasi tu wake: tu watu wake, tu kondoo za malisha yake.
    Ingieni malangoni mwake kwa shukrani, nyuani mwake kwa sifa : mshukuruni, mlibarikie jina lake.
    Kwani Yehova ndiye mwema, ni za milele ihisani zake : uaminifu wake wafikilia vizazi vyote.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana : na kwa Roho Mtakatifu:
    Kama vile mwanzo, na sasa : hata milele ni vivyo. Amina.

Hapo huimbwa au husomwa Imani ya Mitume na yule Padre na wale watu, hali wote wamesimama: isipokuwa haisomwi Imani hii siku hizo ambazo imeagizwa kusomwa Imani ya Mtakatifu Athanasio.
 

Psalm 100

NAAMINI kwa Mungu Baba, Mwenyezi, Muumbambingu na nchi:
    Na kwa Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu, ambaye alitungishwa mimba na Roho Mtakatifu, Akazaliwa na Mwanamwali Mariamu, Akateswa katika enzi ya Pontio Pilato, Akasalibiwa, akafa, akazikwa, Akashuka na kuingia kuzimu; Hata siku ya tatu akasimama tena, ametoka kwa wafu, Akapaa na kuingia mbinguni, Naye ameketi upande wa mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu, Baba; Ndiko atakakotoka, kuja kuwaarnua walio hai hata waliokufa.
    Naamini kwa Roho Mtakatifu; na Kanisa Takatifu lililo ulimwenguni mote; na. Ushirika wa Watakatifu; na Madhambi kusamehewa; na Mwili kufufuka; na Maisha ya milele. Amina.

Kisha husaliwa Sala hizo zifuatazo hapa, watu hali wamepiga magoti kwa makini; yule Padre hutangulia kutamka kwa sauti kuu,

          Bwana na awe pamoja nanyi.
Huitika. Na awe pamoja na roho yako.
Padre. Na tuombe.

Bwana, uturehemu.
Kristo, uturehemu.
Bwana, uturehemu.

Hapo yule Padre na waimbaji na wale watu husoma Sala ya Bwana kwa sauti kuu.
 

Apostles' Creed

BABAETU uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako na uje. Mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, Kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu. wa kututosha. Nawe utusamehe makosa yetu, Kama nasi tulivyowasamehe watukosao, Nawe usitupe1eke katika kujaribiwa; Utuokoe maovuni. Amina.

Hapo Padre husimama na kusema,

        Ewe Bwana, utuonyeshe rehema yako juu yetu.
    Huitika. Utupe na wokofu wako.
    Padre. Ewe Bwana, umweke salama Mfalme.
    Huitika. Nawe utusikize kwa rehema, wakati tukulinganapo.
    Padre. Uwavike haki watumishi wako.
    Huitika. Uwaweke na furaha wateule wako
    Padre. Ewe Bwana, uwaokoe watu wako.
    Huitika. Ubarikie na urithi wako.
    Padre. Ewe Bwana, utupe amani kwa hizi zaman zetu.
    Huitika. Kwa maana, hakuna mwenye kututetea, asiyekuwa wewe, Mwenyezi Mungu.
    Padre. Ewe Mwenyezi Mungu, utufanye safi mioyo yetu ndani.
    Huitika. Wala usituondolee Roho wako Mtakatifu.

Hapo hufuata Sala tatu: ya Kwanza ni ya Siku ile, maana, ni ile ile iliyoamriwa katika Ushirika: ya Pili ni ya kuombea Amani: ya Tatu ni ya kuombea Neema ya kuishi vyema. Na Sala mbili hizo za mwisho hazibadiliki, husomwa siku zote wakati wa Sala ya Asubuhi mwaka mzima, kama zifuatanavyo hapa: na wale watu hali wamepiga magoti wote.
 

Lord's Prayer

SALA YA PILI, YA KUOMBEA AMANI

EWE Mwenyezi. Mungu, Mwenye kubuni amani na kupenda mapatano, maisha yetu ya milele ya katika kukujua wewe, kukutumikia wewe ndio uhuru uliokamilika: utukingie sisi watumishi wako wanyenyekevu kila tukifuliwa na adui; ili kwa kutumaini sana ulinzi wako, tusiche nguvu za adui zetu wawao wote, kwa uwezo wa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.
 

2nd Collect, for Peace

SALA YA TATU, YA KUOMBEA NEEMA

EWE Bwana, Babaetu wa mbinguni, Mwenyezi Mungu, Mkazi wa milele, uliyetufikisha katika mwanzo wa siku hii salama; utuhifadhi leo kwa nguvu zako zisizowezekana ; nawe ukubali ya kwamba siku hii tusiangukie katika dhambi, wala kuingia katika hatari kwa neno lolote; bali iwe vitendo vyetu vyote kuamrishwa na uongozi wako, hata tukafanye daima yaliyolekea machoni mwako; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

Katika maimbio na penye waimbaji, hapa huletwa Wimbo.

Kisha hapo husomwa Sala hizi tano zifuatazo, isipokuwa wakati isomwapo Litania: na wakati huo, sala zisomwazo ni hizo mbili za mwisho, kama vile zilivyowekwa hapo.
 

 
3rd Collect, for Grace

SALA YA KUMWOMBEA MTUKUFU MFALME

EWE Bwana, Babaetu wa mbinguni, mtukufu, mweza, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana, Mtawalamaseyidi pekeo, nawe huko uliko kitini mwako unawaangalia watu wote pia wakaao duniani; sisi twakuomba sana umwangalie kwa neema yako Bwana wetu Sultani mwenye ihisani, Mfalme GEORGE; umwongeze sana neema hiyo ipatikanayo kwa Roho wako Mtakatifu, hata awe siku zote kuyashika uyapendayo wewe, na kwenenda umlekezako: umvike vipawa vyako vya mbinguni kwa wingi; umkirimu kuishi sana kwa afya na uwezo; umtie nguvu apate kuwashinda na kuwapita adui zake wote; na baada ya haya, kisha, afikilie furaha na baraka zisizokoma; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.
 

 
Prayer for the King's Majesty

SALA YA KUWAOMBEA WATU WA JAMAA YA UFALME

EWE Mwenyezi Mungu, shina la wema wote, sisi twakuomba sana kwa unyenyekevu umbarikie mkewe mfalme wetu, Bibi Elizabeth mwenye fadhili, na Bibi Mary mamaake mfalme, na Princess Elizabeth, na jamaa wote wa Ufalme: uwavike Roho wako Mtakatifu; uwaneemeshe neema yako ya mbinguni; uwafanishe kwa raha yote; uwafikishe na katika ufalme wako wa milele; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.
 

Prayer for the Royal Family

SALA YA KUWAOMBEA MAPADRE WA KANISANI NA WATU WAO

EWE Mwenyezi Mungu, Mkazi wa milele, kila miujiza bora hakuna mwenye kuifanya isipokuwa wewe; twawaombea mabishopu wetu na watunzao roho za watu, na vikao vyote vya watu walivyopewa hao kuvitunza, ya kwamba uwashushie Roho wako, ambaye ni Mpaji wa neema. yako; kisha, ili kwamba watu hao wakupendeze kweli, uwamiminie umande usiokoma wa baraka yako. Utupe haya, twakuomba, Bwana, kwa ajili ya heshima ya Msaada wetu, Mwombezi wetu, Yesu Kristo. Amina.
 

Prayer for Clergy & People

SALA YA MTAKATIFU CHRYSOSTOM

EWE Mwenyezi Mungu, uliyetupa neema sisi kwa wakati huu kukuletea wewe maombi yetu sote pia kwa nia moja; nawe ndiwe mwenye kutoa ahadi ya kwamba, watu wawili watatu watakapokutanika pamoja kwa jina lako, utawapa wakutakayo: ututimizie sasa, Bwana, haja zetu na sala zetu watumishi wako, kwa jinsi yatakavyotufaa; kwa kutupa kuijua kweli yako katika ulimwengu huu, na maisha ya milele katika ulimwengu ujao. Amina.

2 Wakorintho 13. 14

NEEMA ya Bwana wetu Yesu Kristo, na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu, viwe pamoja nasi sote milele. Amina.

Taratibu ya Sala ya Asubuhi ya kila siku mwaka mzima imekoma hapa

Prayer of St. Chrysostom

 

Return to the 1662 Book of Common Prayer in Swahili

Web author: Charles Wohlers U. S. EnglandScotlandIrelandWalesCanadaWorld