The Book of Common Prayer
United States England Scotland Ireland Wales Canada World

    Chuo cha Sala ya Umoja (1662)
The 1662 Book of Common Prayer in Swahili

 

TARATIBU YA NDOA

Watu wote watakaooa na kuolewa hutangulia kuitangaza habari ya ndoa yao msikitini siku za Jumapili tatu mbali mbali, wakati wa Sala ya Asubuhi, au, (ikiwa hakuna Sala ya Asubuhi,) wakati wa Sala ya Jioni : yule Padre hunena kama taratibu ya desturi,
 

Marriage

MIMI naitangaza habari ya ndoa kati ya Fulani, mtu aketiye pahali fulani na Fulani mwanamke aketiye pahali fulani. Pakiwa na mtu kwenu ajua sababu au kizuizi cha haki cha kuwazuia watu hawa wawili wasiungamanishwe katika Ndoa takatifu, imempasa kusema.
    Hii ndiyo mara ya kwanza, (au ya pili, au ya tatu), ya kuwauliza kama haya.

Na wakiwa wakaa katika mipaka ya misikiti mbali mbali, hutolewa maulizo ya habari yao katika misikiti yote miwili, yule Padre wa msikiti huu na asiwaoze asipopata hati ya kumpa hakika ya kuwa yamekwisha kuulizwa maulizo mara tatu, nayo hati hiyo huipata kwa Padre yule wa msikiti ule wa pili.

Siku iliyoagizwa kuwaoza wale wawili ikifika saa yake, yule atakayeoa na yule atakayeolewa, huingia ndani ya msikiti pamoja na rafiki zao na jirani zao, wasimame pamoja wale wawili, yule mwanamume upande wa mkono wa kuume na yule mwanamke upande wa mkono wa kushoto: ndipo hunena yule Padre,

ENYI mpendwao sana, tumekutana hapa mbele za Mwenyezi Mungu na mkutano huu, tupate kuwaungamanisha mwanamume huyu na mwanamke huyu katika Ndoa takatifu, nayo ni hali moja iliyowekwa na Mwenyezi Mungu zamani walipokuwa watu hawajafanya makosa, tena yatuonyesha ule umoja ulio wa siri alio nao Kristo na kanisa lake: nayo hali hiyo iliyo takatifu sana Kristo aliiheshimu na kuitia uzuri, kwa vile alivyokwenda arusini yeye mwenyewe, na kwa ishara yake ya kwanza aliyoitenda katika Kana ya Galilaya; kisha yasifiwa hali hiyo na mtakatifu Paulo kuwa ni hali ya kuheshimiwa na watu wote; na kwa ajili ya hayo imekuwa haifai kujitia wala kuingia kwa upesi na pasipo kuifikiri wale wenyewe, ili kutimiza tamaa na shauku zao za miili yao, wakawa mfano wa nyama wasiokuwa na akili. Basi waiingiao na waingie kwa ustahivu, kwa busara na mashauri na kwa makini na kumcha Mungu, huku wayafikiri ni kwa maana gani hata yakawekwa na Mwenyezi Mungu haya mambo ya Ndoa.
    Kwanza: yaliwekwa kwa maana ya kuzaa wana, wapate kulewa hao katika kicho cha Bwana na ulezi wake; na kulivutia sifa jina lake lililo takatifu.
    Pili: yaliwekwa ili yapate kuwa dawa ya dhambi, ili watu wapate kujitenga na uzinifu, na kwamba hao ambao kwamba kile kipawa cha kujizuia hawanacho wapate kuoa, na kujiweka hali ya kuwa via visivyo na najisi vya mwili wa Kristo.
    Tatu: yaliwekwa kwa ajili ya wenyewe kufungamana na kusaidiana na kutunzana, kama ambavyo yampasa huyu kuvipata kwake huyu katika mambo ya maisha yao, katika kufanikiwa na katika shida: nao watu hawa wawili waliopo sasa wamekuja kuungamanishwa katika hali hiyo iliyo takatifu. Basi, akiwa mtu aweza kuonyesha sababu ya haki iwayo yote itakayowazuilia kuungamanishwa pamoja kwa halali, na aiseme sasa, au tokea sasa milele anyamaze.

Kisha baadaye husema na wale watakaoozwa, akinena,

MIMI nawaonya na kuwaamuru ninyi nyote wawili, kwa mtakavyohukumiwa katika siku kuu ya hukumu, ambayo ni ya kutisha sana, napo ndipo zitakapofunuliwa siri za mioyo ya watu wote, ya kwamba, akiwa mmoja katika ninyi wawili amejua kizuizi kitakachowazuia ninyi wawili kuungamanishwa katika Ndoa kwa halali, muungame hivi sasa kizuizi hicho na kukifunua. Kwani jueni sana ya kwamba kadiri ya waungamanishwao kwa jinsi isivyoambiwa kuwa halali na Neno lake Mwenyezi Mungu, hawaungamanishwi watu hao na Mwenyezi Mungu, wala Ndoa zao si halali.

Na siku ya ndoa ·hizo, akiwa mtu awaye yote yuashuhudia na kuonyesha kizuizi chochote, kitakachowazuia kuungamanishwa katika ndoa kama ilivyoagizwa na sheria ya Mungu au ya Ufalme huu, naye mtu yule yu tayari kutoa dhamana na madhamini wengine pamoja naye, ambao ni wa kutosha katika hayo, kwao watakaooana; au aweke rahani kwa thamani iliyotimia ya gharama walizogharimishwa wale watakaooana, ili apate kuyathubutisha kuwa kweli ayashuhudiayo, ndipo hapo, yalazimu kutaaharisha kule kuzipisha ndoa zao watu wawili wale, hata iishe kuangaliwa ile kweli.

Na ikiwa hakikusemwa kizuizi kiwacho chote, ndipo hapo yule Padre humuulizayule mtu mume,
 

Banns

EWE Fulani, umependa uwe naye mwanamke huyu, kuwa mkeo wa kumwoa, mwishi wewe naye kama maagizo ya Mwenyezi Mungu, katika hali takatifu ya Ndoa? Utampenda, utamtuliza moyo wake, na kumstahi, na kumtunza, akiwa hawezi, akiwa mzima; na wengine wote utawaepuka, ujiweke wewe kuwa na yeye muda wote mtakaokuwa hai pamoja duniani?

Yule mume hujibu,

Nakubali.

Ndipo hapo yule Padre humuuliza yule mwanamke,

EWE Fulani, umependa uwe naye mtumume huyu kuwa mumeo wa kukuoa, mwishi pamoja kama maagizo ya Mwenyezi Mungu katika hali takatifu ya Ndoa? Utamtii na kumtumikia, utampenda na kumstahi na kumtunza, akiwa hawezi, akiwa mzima; na wengine wote utawaepuka, ujiweke wewe kuwa naye muda wote mtakaokuwa hai pamoja duniani?

Yule mke hujibu,

Nakubali.

Ndipo hapo yule Padre hunena,

Ni nani amtoaye mwanamke huyu ili kumwoza mume huyu?

Ndipo watakapoapiana yamini kama hivi: yule Padre humpokea yule mwanamke mikononi mwa babaye, au rafikiye, na kumfanya yule mume, kwa mkono wake yeye wa kuume, amshike mkono wake wa kuume yule mwanamke, akimfunza kusema,
 

Questions of bride & groom

MIMI Fulani nakutwaa wewe Fulani kuwa mke wangu wa kukuoa, niwe nawe nikushike toka hii siku ya leo, kwa wema kwa ubaya, kwa wingi wa mali kwa uchache wa vitu, katika ugonjwa katika afya, nikupende na kukutunza hata kufa, kama amri zake takatifu Mwenyezi Mungu. Nami kwa ajili ya neno hili nakupa yamini yangu.

Ndipo hapo huachana mikono, kisha baadaye yule mwanamke kwa mkono wake wa kuume humshika yule mume mkono wake wa kuume, na kunena naye kwa kufuata yule Padre,

MIMI Fulani nakutwaa wewe Fulani kuwa mume wangu wa kunioa, niwe nawe nikushike toka hii siku ya leo, kwa wema kwa ubaya, kwa wingi wa mali kwa uchache wa vitu, katika ugonjwa katika afya, nikupende na kukutunza na kukutii hata kufa, kama amri zake takatifu Mwenyezi Mungu. Nami kwa ajili ya neno hili nakupa yamini yangu.

Ndipo hapo huachana mikono mara ya pili, yule mume humpa yule mke pete, akiiweka juu ya Chuo, pamoja na ada, kama walivyozoea kupewa Padre na katibu wake. Yule Padre akiisha kuitwaa ile pete humpa yule mume, yule mume apate kumvika yule mwanamke kidole cha nne cha mkono wa kushoto; kisha yule mume huishika ile pete hapo, na kunena kwa kufunzwa na yule Padre,

MIMI kwa pete hii nakuoa, kwa mwili wangu nakuheshimu, nami nakupa vitu vyangu vyote vya duniani: kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.

Ndipo hapo yule mume huiacha ile pete katika kidole cha nne cha mkono wa kushoto wa yule mwanamke, kisha wakipiga magoti wote wawili, yule Padre hunena,

Na tuombe.

EWE Mwenyezi Mungu, huna mwanzo huna mwisho; Muumba wa wanadamu wote ni wewe, nawe ndiwe mwenye kuwatunza; wewe watupa kila neema ya rohoni; ndiwe mwenye kuanziza maisha yasiyo ukomo: uwateremshie baraka yako hawa watumishi wako, mtumume huyu na mwanamke huyu, ambao sisi twawaombea hivi kwa jina lako; ili kwamba kama walivyoishi pamoja Isaka na Rebeka kwa uaminifu, watu hawa nao washike vivyo kuondoa na kutimiza yamini zao na maagano waliyowekeana, ambayo pete hii waliyopanana na kupokeana hivi ndiyo dalili yake na sahihi yake; nao wadumu daima katika umoja wa mapenzi na amani vilivyo timia, waishi kwa kufuata sheria yako; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

Ndipo hapo yule Padre huwashikamanisha mikono yao ya kuume, huyu na huyu, na kunena,

ALIOWAUNGAMANISHA Mwenyezi Mungu, binadamu na asiwatenganishe.

Ndipo hapo yule Padre husema na wale watu,

KWA maana ya kuwa Fulani na Fulani wamekubaliana katika Ndoa takatifu; nao neno hilo wamekiri mbele za Mwenyezi Mungu na mkutano huu, tena wamepanana yamini, wameapiana wenyewe kwa wenyewe, nayo wameiweka wazi na kuikiri mbele ya watu kwa kutoa na kupokea pete na kushikana mikono; mimi nasema hawa ni mume na mkewe pamoja, kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.

Yule Padre huongeza na maneno haya ya Baraka,
 

The Marriage

MUNGU Baba, Mungu Mwana, Mungu Roho Mtakatifu, na awabarikishe, awalinde na kuwaweka salama; Bwana na awaangalie kwa rehema zake na kuwaneemesha, na kwa mtakavyojawa na baraka za rohoni na neema pia kwake yeye, muwe watu wa kukaa pamoja kwa wema katika maisha haya, wenyewe kwa wenyewe, hata katika ulimwengu ujao myapate maisha yasiyo mwisho. Amina.

Ndipo hapo yule Padre au wale wenye daraja, hwenda katika Meza ya Bwana, na kunena au kuimba Zaburi hii inayofuatana hapa.

Beati Omnes. Zaburi 128

YUNA heri kila mtu amchaye Yehova: aendaye katika njia zake.
    2. Taabu ya mikono yako hakika utaila: utakuwa na heri, na kwako kwema.
    3. Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao vyumbani mwa nyumba yako: wanao kama vichipukizi vya mizeituni wakiizunguka meza yako.
    4. Hivyo ndivyo atakavyo barikiwa : mtu yule amchaye Yehova.
    5. Yehova akubarikie toka Zayuni: upate kuyaona mema ya Yerusalemu siku zote za maisha yako.
    6. Naam, ukawaone wana wa wanao: amani na iwe juu ya Isiraeli.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu;
    Kama vile mwanzo, na sasa: hata milele ni vivyo. Amina.

Au Zaburi hii,

Deus Misereatur. Zaburi 67

MUNGU na atufanyie fadhili, atubarikie: na atufikizie nuru za uso wake kwetu :
    2. Ili njia yako itamburikane juu ya nchi: wokofu wako ujulikane katika mataifa wote.
    3. Watu na wakushukuru wewe, Mungu: watu wote pia na wakushukuru wewe.
    4. Mataifa na wafurahi, waimbe kwa furaha: kwa kuwa wewe utawahukumu watu haki, utawaongoza mataifa walio duniani.
    5. Watu na wakushukuru wewe, Mungu: watu wote pia na wakushukuru wewe.
    6. Nchi na itoe mazao yake: Mungu, Mungu wetu, na atubarikie,
    7. Mungu atatubarikia: ncha zote za dunia na zimche yeye.
    Utukufu uwe kwa Baba, na kwa Mwana: na kwa Roho Mtakatifu ;
    Kama vile mwanzo, na sasa: hata milele ni vivyo. Amina.

Baada ya kwisha ile Zaburi, yule mtu na yule mke hupiga magoti mbele ya Meza ya Bwana, yule Padre husimama mbele ya Meza na kuwalekea, na kunena,

Bwana, uturehemu.

Huitika. Kristo, uturehemu.
Padre. Bwana uturehemu.
 

Blessing

BABAETU uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako na uje, Mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, Kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kututosha. Nawe utusamehe makosa yetu, Kama nasi tulivyowasamehe watukosao. Nawe usitupeleke katika kujaribiwa, Utuokoe maovuni. Amina.

    Padre. Ewe Bwana, uwaokoe mtumwa wako na kijakazi chako,
    Huitika. Waliokutumaini wewe.
    Padre. Ewe Bwana, uwaletee msaada kutoka katika pahali patakatifu pako;
    Huitika. Uwalinde milele.
    Padre. Uwe kwao ukuta wenye imara,
    Huitika. Kuwakinga na uso wa adui zao.
    Padre. Ewe Bwana, utusikize maombi yetu;
    Huitika. Kilio chetu kikufikilie uliko.
    Padre. Ewe Mungu wa Iburahimu, nawe u Mungu wa Isaka, tena u Mungu wa Yakobo, uwabarikie hawa watumishi wako; nawe uipande mbegu ya maisha ya milele mioyoni mwao, ili watakalojifunza lolote katika Neno lako takatifu, walitimize halisi. Nawe huko uliko mbinguni uwaangalie kwa wema uwabarikie. Nawe kama vile ulivyowateremshia baraka yako Iburahimu na Sara, kwa kuwatuliza sana, na hawa watumishi wako nao uwafadhili kwa kuwateremshia baraka yako vivile; hata, kwa watakavyoyatii mapenzi yako wewe, na kukaa salama daima katika ulinzi wako, iwe wao kudumu mumo katika kupendana na wewe, hata maisha yao ya huku yaishe; kwa Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.

Sala hiyo ifuatanayo huachwa awapo yule mwanamke si mtu wa kuchukua mimba tena.

EWE Bwana mwenye rehema, Babaetu wa mbinguni, ni kwa vipawa vyako vya neema binadamu waongezekavyo; sisi twakuomba kwamba uwasaidie watu wawili hawa kwa kuwabarikia, hata iwe wao kuwa watu wa baraka katika kuzaa wana, nao wawe watu wa kukaa pamoja kwa kupendana kwa uaminifu, hata iwe wao kuwaona wana wao wenye kulewa katika imani ya Kristo na adili, kwa kukutukuza na kukuheshimu; kwa Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

EWE Mwenyezi Mungu, wewe kwa nguvu za uwezo wako ulifanya vitu vyote pasi kitu chochote; tena, (baada ya kwisha kutengea yale mengine), ukaamuru kwa yule mtu mume Adamu (yule uliyemuumba kwa mfano wa sura zako wewe), ipatikane asili ya yule mwanamke, ikawa ndio mwanzo wake; nawe, kwa vile ulivyowaungamanisha wale wawili ukafunza kana kwamba hao uliokwisha kuwaungamanisha pamoja kwa ndoa, haitakuwa halali kuwatenganisha popote: ewe Mwenyezi Mungu, uliyeitakasa hali hiyo ya ndoa ikawa ni siri tukufu sana kwa jinsi ambavyo ndani yake zimefananishwa na kufunuliwa ndoa na umoja vya rohoni, vilivyo kati yake Kristo na kanisa lake; uwaangalie. kwa rehema hawa watumishi wako, ili kwamba huyu mume ampende mkewe kwa mfano wa Neno lako (vivile kama Kristo alivyompenda mposwa wake, nalo ni kanisa, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake, kwa kulipenda na kulilea, vivile kama mtu apendavyo mwili wake); tena na kwamba huyu mke naye awe mwenye kupenda na kupendekeza, kwa uaminifu na usikizi, kwa mumewe, kwa kuwaandama watuwake wote wamchao Mungu, kwa utulivu na makini na imani.
    Ewe Bwana, uwabarikie wao wote wawili, uwape na kuurithi ufalme wako wa milele, kwa Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.

Ndipo hapo hunena yule Padre,

MWENYEZI Mungu, aliyewaumba hapo kwanza wazazi wetu wa asili, Adamu na Hawa, akawatakasa na kuwaungamanisha pamoja katika ndoa, na awamiminie juu yenu mali ya neema yake, awatakase na kuwabarikia, ili kwamba mpendekeze kwake, huku katika miili yenu na huku katika roho zenu, nanyi mwishi pamoja katika mapenzi matakatifu hata maisha yenu yaishe. Amina.

Baada ya kwisha sala hizi, ikikosekana hotuba ya kufunua yaliyowapasa mtu na mkewe, yule Padre husoma haya:
 

Lord's Prayer

ENYI nyote mliooa au kuolewa, au mlio na azima ya kuingia katika hali takatifu ya Ndoa, sikizeni yanenwayo na Maandiko matakatifu katika yaliyowapasa wale waume kwa wake wao, na wale wake kwa waume wao.
    Mtakatifu' Paulo katika Waraka wake aliowapelekea Waefeso, Mlango wa tano, yuawaagiza maagizo haya waume wote waliooa wake: Ninyi waume, wapendeni wake wenu, vivile kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, na kutoa nafsi yake kwa ajili yake: ili kwamba apate kulitenga, akiisha kulisafi kwa kuosha kwa maji katika neno, ili kwamba aipatie nafsi yake kanisa tukufu, lisilo na kipaku wala alama ya mkuto, wala neno lolote kama paya: lakini ya kwamba liwe takatifu pasipokuwa na aibu. Ni vivyo hivyo imewapasa watu waume nao kuwapenda wake wao kama vile waipendavyo miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe huipenda nafsi yake: kwani hapana mtu aliyeichukia nyama ya mwili wake popote: lakini ni kuilisha na kuienga-enga, vivile kama Kristo naye alivyolitunza kanisa: kwa kuwa sisi tu via vya mwili wake, vya nyama yake na vya mifupa yake. Kwa ajili ya hayo mtu atawaacha babaye na mamaye, naye ataambatana na mkewe, nao hao wawili watakuwa ni mwili mmoja. Siri hii ni siri kuu: ila mimi naleta habari ya Kristo na hilo kanisa. Pamoja na hayo, na ninyi kila mtu nafsi yake na ampende mkewe mwenyewe kama nafsi yake.
    Naye yeyule mtakatifu Paulo, akiwaandikia Wakolosai anena hivi na waume wote waliooa; Enyi waume, wapendeni wake wenu, msiwaonee machungu.
    Msikizeni na aliyoyanena mtakatifu Petero, mtume wake Kristo, naye ni mtu aliyeoa mke, awaambiapo waliooa: Nanyi waume, ni vivyo hivyo, ketini na wake wenu sawasawa ha kujua kwenu, kwa kumpa mwanamke heshima impasayo, kama chombo kilicho kinyonge zaidi ya ninyi, tena kama mlivyokuwa warithi pamoja wa neema ya uhai; ili kwamba kuomba kwenu kusizuiliwe.
    Haya mliyoyasikia hivi ni yampasayo yule mume kwa mkewe. Basi nanyi wake kadhalika sikizeni yawapasayo kwa waume wenu, nayo yameonyeshwa wazi katika Maandiko matakatifu.
    Mtakatifu Paulo katika Waraka ule ule aliowape1ekea Waefeso tuliotaja huku mbele, huwafunza ninyi kama haya: Ninyi wake, nyenyekeeni kwa waume wenu, kama vile kwa Bwana. Kwa kuwa mtu mume ni kichwa cha mwanamke, vivile kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa, mwenyewe ni mwokozi wa mwili. Lakini kama kanisa lilivyomnyenyekea Kristo, ni vivyo hivyo na wanawake wawe kwa waume wao katika mambo yote. Naye anena tena, Huyo mwanamke naye na aangalie ya kwamba amche mumewe. Naye katika Waraka wake aliowapelekea Wakolosai mtakatifu Paulo huwafunza haya yaliyo mafupi, Enyi wake, nyenyekeeni kwa waume wenu, kama vifaavyo katika Bwana.
    Mtakatifu Petero naye huwafunza vyema sana anenapo kama haya: Enyi wanawake, jiwekeni nafsi zenu chini ya waume wenu wenyewe; ili kwamba, ikiwa wengine wako wasiolitii hilo neno, wapatikane kwa njia ya miendo ya hao wake wao, pasipokuwa na lile neno; wakiutunza kwa macho yao ule mwendo wenu ulio safi, ulio wa hofu. Ambao, kujipamba kwenu kusiwe kule kujipamba kwa nje kwa kusonga nywele, na kuvaa vyombo vya dhahabu, au kujivika nguo; lakini na kuwe mtu aliyefichamana wa moyoni, katika mavao hayo yasiyoharibika, maana, ni yale ya roho ya upole na utulivu, roho ambayo mbele za Mwenyezi Mungu ina thamani kuu. Kwani hao wanawake watakatifu nao hapo kale, hao walio tumaini kwa Mungu, ndivyo walivyozipamba nafsi zao, na kunyenyekea kwa waume wao wenyewe: kama Sara alivyomtii Iburahimu, akimwita bwana: nanyi mu watoto wake huyo, mkifanya yaliyo mema, nanyi hamtishwi kwa hofu yoyote.

Yafaa, wale waliooana upya washirikiane Ushirika Mtakatifu zamani za kuoa, au mara watakapowahi baada ya kuoana.
 

Exhortation

Kama hapana Ushirika Mtakatifu wala hotuba ya kuonyesha yawapasa yo mume na mkewe, na lisomwe fungu la Maandiko matakatifu ; au yule Padre aseme maonyo yaliyo katika Chuo cha Sala cha tangu hapo. Ndipo yule Padre huwafumua wale watu waliokutanika, akisema,

Na tuombe.

EWE Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa milele, twakuomba uone vyema kutuongoza, na kututakasa, na kututawala, mioyo yetu na miili yetu, katika njia za sheria zako, na katika kazi za maagizo yako; ili kwa kulindwa na wewe kwa nguvu zote, hapa na hata milele, tuhifadhike miili yetu na roho zetu, kwa Bwana wetu, Yesu Kristo. Amina.

BARAKA ya Mungu, Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, iwe mwenu, ikae kwenu daima. Amina.

This appears to be the dismissal from the end of the C of E 1928 Marriage Service

 

Return to the 1662 Book of Common Prayer in Swahili

Web author: Charles Wohlers U. S. EnglandScotlandIrelandWalesCanadaWorld