MAJIBIZANO
(au Katekisimo)
Nayo ni mafunzo ya kujifunza kila mtu kwanza
asijaletwa kwa Bishopu ili kuthubutishwa,
A. humuuliza B.
Jina lako nani?
B. humjibu A.
Jina langu mimi ni (jina la Kikristo).
A. Jina hilo ulipewa na kina nani?
B. Jina hilo walionipa ni madhamini wangu, hapo katika ubatizo wangu; nami katika jambo hilo nilifanywa kuwa kia cha Kristo, na kuwa mtoto wake Mwenyezi Mungu, na kuwa mtu wa kuurithi ufalme wa mbingu.
A. Ni neno gani walilokufanyia madhamini wako wakati huo?
B. Walifanya mambo matatu kuyaahidi na kuyaweka nadhiri kwa jina langu mimi. La kwanza, ni la mimi kumkataa Shetani na kazi zake zote, na furaha ya ulimwengu huu na upuzi wake, na shauku zote za mwili zilizo na dhambi. Pili, kuwa nitaziamini Sharti zote za Imahi ya Ukristo. Tatu, kuwa nitayashika mambo matakatifu ya mapenzi yake Mwenyezi Mungu na maagizo yake, na kuyaandama mambo hayo siku zote nitakazokuwa hai duniani.
A. Je, huoni moyoni mwako kuwa umelazimiwa na kuyaamini hayo waliyoyaahidi kwa jina lako, na kuyatenda?
B. Hakika yangu ndiyo nionayo: nami kwa msaada wake Mwenyezi Mungu nitatenda vivyo. Nami ndani ya moyo wangu namshukuru Babaetu wa mbinguni kwa vile alivyoniita na kuniweka hali hii ya wokofu kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Nami namwomba Mwenyezi Mungu anipe neema yake, nipate kudumu mumu humu hata mwisho wa maisha yangu.
A. Sema Sharti za Imani yako. |
B. Naamini kwa Mungu Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na nchi; na kwa Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu; ambaye alitungishwa mimba na Roho Mtakatifu: akazaliwa na Mwanamwali Mariamu; aka-teswa katika enzi ya Pontio Pilato; akasalibiwa, akafa, akazikwa; akashuka na kuingia kuzimu : hata siku ya tatu akasimama tena, ametoka kwa wafu. Akapaa na kuingia mbinguni; naye ameketi upande wa kuume wa Mwenyezi Mungu, Baba. Ndiko atakakotoka kuja kuwaamua walio hai hata waliokufa.
Naamini kwa Roho Mtakatifu; na Kanisa takatifu lililo ulimwenguni mote; na Ushirika wa watakatifu; na Madhambi kusamehewa; na Mwili kufufuka; na Maisha ya milele. Amina.
A. Katika hizi Sharti za Imani yako ni mambo gani ujifunzayo sana?
B. Mimi kwanza hujifunza niamini kwa Mwenyezi Mungu Baba, aliyeniumba mimi na ulimwengu wote pia.
Pili, niamini kwa Mungu Mwana, aliyenikomboa mimi na wanadamu wote.
Tatu, niamini kwa Mungu Roho Mtakatifu, anitakasaye mimi na wateule wake Mwenyezi Mungu pia wote.
A. Ulisema kwamba madhamini wako waliahidi kwa ajili yako, ya kuwa utayashika maagizo yake Mwenyezi Mungu; maagizo hayo niambie ni mangapi hesabu yake?
B. Ni kumi. |
Apostles' Creed |
A. Ni kama yapi?
B. Ni kama aliyoyasema Mwenyezi Mungu katika Chuo cha Exodus, Mlango wa Ishirini, aliponena, Mimi ni Yehova Mwenyezi Mungu wako, niliyekutoa nchi ya Misri, kutoka hiyo nyumba ya utumwa.
I. Usiwe na miungu mingine mbele zangu wawao wote.
II. Usifanye sanamu ya kuchonga, umbo lolote lililo juu mbinguni, au lililo chini duniani, au lililo chini ya dunia katika maji: usivisujudie, wala kuvitumikia: kwa kuwa mimi Yehova Mungu wako ni Mungu mwenye wivu, niwapatilizaye wana kwa uovu wa baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao; na kuwapa rehema watu elfu elfu wanipendao, wayashikao maagizo yangu.
III. Usitaje jina la Yehova Mungu wako kwa upuzi, kwani Yehova hatamfanya kuwa hana makosa mtu atajaye jina lake kwa upuzi.
IV. Ikumbuke siku ya sabatu kuitakasa. Siku sita tumika, ufanye kazi zako zote; ila siku ya saba ndiyo sabatu ya Yehova Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi, wewe, wala mwanayo mume na mke; wala mtumwayo mume na mke; wala nyama zako za mji; wala mgeni wako aliye ndani ya malango yako: maana, kwa siku sita Yehova alifanya mbingu na nchi, na bahari, na vyote vilivyo humo, akapumzika kwa siku ya saba: ndipo akaibarikia Yehova ile siku ya sabatu, akaitakasa.
V. Mheshimu babaako na mamaako, siku zako zifanyike ndefu juu ya nchi upewayo na Yehova Mungu wako.
VI. Usiue.
VII. Usizini.
VIII. Usiibe.
IX. Usimshuhudie mwenzio kwa uwongo.
X. Usitamani nyumba ya mwenzio, usimtamani mke wa mwenzio ; wala mtumwawe, mume au mke; wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kiwa cho chote alicho nacho mwenzio.
A. Ujifunzayo sana katika maagizo haya ni mambo gani?
B. Mimi nijifunzayo sana ni mambo mawili': yaliyonipasa kwa Mwenyezi Mungu, na yaliyonipasa kwa mwenzangu.
A. Je, yaliyokupasa kwa Mwenyezi Mungu ni yapi?
B. Mimi yaliyonipasa kwa Mwenyezi Mungu ni kumwamini na kumcha na kumpenda, kwa moyo wangu wote, na akili zangu zote, na roho yangu yote, na nguvu zangu zote; na kumwabudu, na kumshukuru, na kutegemea kwake kabisa; na kumlingana, na kumheshimu jina lake takatifu na Neno lake, na kumtumikia kweli siku zote niishizo.
A. Yaliyokupasa kwa mwenzio ni yapi?
B. Yaliyonipasa kwa mwenzangu ni kumpenda kama nafsi yangu, na watu wote kuwatendea vyema kama ambavyo mwenyewe ningependa nitendewe na wao: ni kuwapenda babaangu na mamaangu, na kuwastahi na kuwasaidia: na kumstahi na kumtii Mfalme, na wote waliowekwa na amri chini yake: na kujinyenyekeza chini ya walio na amri juu yangu, na waalimu wangu, na wanichungao roho, na bwana zangu, jamii ya walioko: na wanipitao kwa madaraja yao kuwakalia kwa unyenyekevu na ustahivu: nisimdhuru mtu awaye yote, katika kutenda wala katika kunena; bali niwe mtu wa kweli na haki katika niyatendayo yote: tena niwe mtu nisiyemwekea mwenzangu mfundo moyoni, wala kumchukia mtu awaye yote: tena niwe mtu mwenye kuizuia mikono yangu na kuiba kitu chochote, na kujilinda ulimi wangu nisiseme maneno mabaya na uwongo, wala nisimsingizie mtu awaye yote: na kujilinda mwili wangu ili nikae hali ya kudhibiti nafsi yangu, na kujilinda na makuu na mambo mabaya ya ulevi na kuzini: tena ni kuwa mtu nisiyetamani mali ya mtu wala kuyalilia choyo; bali niwe mwenye kujifunza na kujibidiisha kufanya kazi yangu nipate riziki zangu, nipate na kutenda yaliyonipasa katika daraja la maisha Mwenyezi Mungu atakayopenda kuniweka, iwayo yote.
Yule Mwalimu huendelea kuuliza,
A. Mwanangu mwema, neno hili moja fahamu sana, ya kwamba mambo haya huyawezi pekeo kuyatenda, wala kwenenda katika maagizo yake Mwenyezi Mungu na kumtumikia, usipopata neema yake. Nayo imekupasa kujifunza kumtaka neema hiyo kila wakati kwa bidii nyingi. Haya basi, nataka kuisikiza Sala ya Bwana, waweza kuisema au huwezi?
|
Questions on Ten Commandments |
Hujibu
B. Babaetu uliye mbinguni, jina lako litakaswe, ufalme wako na uje, mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kututosha. Nawe utusamehe makosa yetu, kama nasi tulivyowasamehe watukosao. Nawe usitupeleke katika kujaribiwa, utuokoe maovuni; kwa kuwa ufalme, na nguvu, na utukufu, ni vyako milele. Amina.
A. Katika sala hii ni neno gani ulitakalo kwake Mwenyezi Mungu?
B. Mimi katika sala hii nataka kwa Mwenyezi Mungu Bwana wangu, Babaetu wa mbinguni, ambaye ndiye mpaji wa kila wema, aniletee mimi neema yake na watu wote, ili tupate kumwabudu na kumtumikia na kumtii, kama itupasavyo. Nami naomba mumo kwa Mwenyezi Mungu, atuletee mambo yote yahitajiwayo na roho zetu na miili yetu; na kuturehemu, na kutusamehe makosa yetu; tena kwamba atapendezewa na kutuokoa na mambo yote yaliyo na hatari, na kutulinda nayo, yakiwa ni ya rohoni au mwilini: naye akubali kutuweka salama na dhambi na kila uovu, na kutuokoa na adui wetu wa rohoni, na mauti ya milele. Nami natumaini nitatendewa hayo na yeye kwa rehema zake na wema wake, kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ndipo nikasema, Amina, maana, na yawe vivile.
|
Lord's Prayer |
Huuliza
A. Ni nyingapi Sakramenti alizoziweka Kristo katika Kanisa lake?
B. Ni mbili tu, ambazo ndizo ziwapasazo watu wote kwa wokofu: nayo ndiyo Ubatizo na Karamu ya Bwana.
A. Waonaje maana yake ni nini hilo jina la Sakramenti?
B. Mimi naona jina la Sakramenti maana yake ni alama ya nje ionekanayo, ya neema ya ndani, ya rohoni, tuliyopewa sisi: nayo alama hiyo ndiyo iliyoagizwa na Kristo mwenyewe, ipate kuwa kama njia ya kuipokelea ile neema, na kuwa buruhani ya hakika ya kuwa nayo.
A. Hii Sakramenti ina mafungu mangapi?
B. Ina mafungu mawili: nayo ni ile alama ya nje ionekanayo, na ile neema ya ndani, ya rohoni.
A. Je, huo Ubatizo, alama yake ya nje ni ipi?
B. Ni maji, ambayo yule mtu. hubatizwa ndani yake, kwa jina Ia Baba, na Ia Mwana, na Ia Roho Mtakatifu.
A. Ile neema ya ndani, ya rohoni, ni ipi?
B. Ni mtu kufa kwa dhambi, akazawa upya kwa haki: kwani sisi kwa ile asili yetu tumezawa katika dhambi, nasi tu wana wa ghadhabu, lakini kwa neema hii sisi kufanywa kuwa wana wa neema.
A. Ni lipi lihitajiwalo kwao watakao kubatizwa?
B. Ni toba, ambayo katika hiyo wao huziacha dhambi: tena imani, ambayo katika. hiyo wao huyaamini sana aliyoyaahidi kwao Mwenyezi Mungu katika Sakramenti hiyo.
A. Basi huwaje kubatizwa wale watoto wachanga, nao wali hali hawawezi kwa ule utoto-uchanga wao kutenda mambo kama hayo?
B. Kwa kuwa walitoa ahadi kuyatenda yote mawili kwa midomo ya wale madhamini wao, na hiyo ahadi yao wakiisha kuwa wakubwa, inawapasa wenyewe kuitimiza.
A. Sakramenti ya Karamu ya Bwana iliagizwa kwa maana gani?
B. Ili kukumbuka daima dhabihu ya kufa kwake Kristo, na kukumbukia zile faida tupatazo humo.
A. Ni lipi fungu la nje la Karamu ya Bwana, maana, ni ipi alama yake?
B. Ni mkate na divai, ambavyo Bwana ameagiza vipokewe.
A. Ni kama lipi lile fungu Ia ndani, maana, ni kama lipi lile jambo lililo onyeshwa maana yake humo?
B. Ni Mwili na Damu yake Kristo, ambazo ni kutwawa na kupokewa hakika hakika pasipo shaka na wale waaminiru, katika Karamu ya Bwana.
A. Ni kama yapi manufaa ambayo tu wenye kuyashirikiana humo?
B. Ni kule kupewa nguvu na kuburudishwa roho zetu kwa Mwili na Damu yake Kristo, kama vivile miili yetu ipewavyo nguvu na ule mkate na ile divai.
A. Hao waiendeao Karamu ya Bwana imewapasa kufanyaje?
B. Waiendeao Karamu ya Bwana imewapasa kupeleleza katika nafsi zao, kujiangalia, ni waliozitubia dhambi zao zilizotangulia au hawakuzitubia, wana na azima iliyo imara ya kuishi maisha mapya na kuwa na imani iliyo hai katika rehema zake Mwenyezi Mungu awarehemuzo katika Kristo, huku wakiyakumbuka mauti yake kwa kushukuru; kisha imewapasa kuketi na watu wote kwa mapenzi.
¶ Katika kila msikiti, yule Padre ndani yake, hujibidiisha kwa siku za Jumapili na za Idi katika Sala ya Jioni katika mwisho wa Somo la pili, kuwafunza na kuwauliza vijana waziwazi mle msikitini, ambao ni wa katika mipaka ya msikiti wake yeye, kama atakavyowaona watosha hesabu yao, maneno ya fungu mojawapo katika mafungu ya majibizano haya.
¶ Na mababa na kina mama, na mabwana na kina bibi kadiri ya waliomo huwaacha wana wao na watumishi wao na wanafunzi wao ambao kwamba hawajajifunza majibizano haya, wapate kwenda msikitini kwa saa iliyowekwa wakamsikize yule Padre kwa kutii hata waishe kujifunza yote ambayo kwamba humu wameagizwa kujifunza.
¶ Na wale wana, mara wakiisha kupata umri wa kufaa, wakajua kuyanena kwa maneno yao waliozawa nayo, maneno ya Imani na Sala ya Bwana na zile Amri kumi, wakajua na kuyajibu mengine yaulizwayo katika majibizano mafupi haya, hapo ndipo wapelekwe kwa Bishopu. Na kila mmoja na awe na mmoja katika madhamini wake kule kushuhudia kuwekewa mikono kwake.
¶ Hata yule Bishopu atakapokwisha kuwajuvisha wenyewe ni wakati gani atakapoletewa vijana kwake wapate kuwekewa mikono, hapo ndipo, wakati huo Padre wa kila msikiti aandike orodha wa majina yao watu hao wote walio katika mipaka ya msikiti wake, ambao kwamba awaona ni watu wa kuletwa kwa Bishopu ili kuthubutishwa, aandike na jina lake mumo, ampelekee au aende nao nafsi yake akampe: na watu hao yule Bishopu atakapowaona wafaa huwawekea mikono kama itakavyoletwa baada ya haya.
|
Questions on Sacraments |
TARATIBU YA KUTHUBUTISHA,
au ya kuwawekea mikono watu ambao kwamba
wamekwisha kufikilia umri wa kupata akili.
¶ Kwa siku waliokwisha kuwekewa wale watu ambao kwamba watathubutishwa wakati huo, huja wakapangwa na kusimama mbele yake yule Bishopu, kisha yeye (au Padre mwingine atakayewekwa na yeye kwa ajili ya neno hili) husoma mwanzo huu wa maelezo wandamao hapa.
ILI kwamba wasongezewe huku kuthubutisha kwa jinsi ya kuwafaa zaidi, hao watakaopewa, Kanisa limeona vyema kuagiza ya kwamba huko mbeleni asithubutishwe mtu ila ajue kuyasema maneno ya Imani yake, na Sala ya Bwana, na zile Amri kumi; ajue na kuyajibu hayo yaliyobaki yaulizwayo katika Majibizano Mafupi: nayo ni ada moja ambayo yafaa sana kuishika; ili kwamba wale watoto wakiisha kukua kuwa watu wenye akili zao, nao wakiisha kujifunza ambayo wale madhamini wao wali-yatoa ahadi kuwafanyia Ubatizo wao, wewe kuyakiri hayo na kuyathubutisha waziwazi mbele ya Kanisa kwa midomo yao na mioyo yao; watoe na ahadi ya wao kwendelea mbele kwa uaminifu katika kujibidiisha kuyatunza, kwa neema yake Mwenyezi Mungu, hayo ambayo kwamba wayaungama kuwa waliyakubali kuyatenda.
|
|
Au huu,
WAPENZI katika Bwana, Kanisa kwa kutumia kuthubutisha hufuata walivyotuonyesha mitume wa, Kristo. Kwa kuwa katika mlango wa nane wa Vitendo vya Mitume twasoma haya:—
Wale waliotawanyika wakazunguka-zunguka wakilihubiri lile neno. Filipu akateremka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri habari njema za Kristo. Walipomwamini Filipu akihubiri ile habari njema ya ufalme wa Mungu na lile jina la, Yesu Kristo, wakabatizwa waume kwa wake. Wale mitume waliokuwa ndani ya Yerusalemu waliposikia ya kwamba Samaria imelipokea neno la Mwenyezi Mungu, wakawapelekea Petero na Yohana; ambao walipokwisha kuteremkia kwao, wakawaombea, ili kwamba wapewe Roho Mtakatifu: kwani hajamshukia mtu wao hata mmoja: isipokuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu. Ndipo wakawekea mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.
Maandiko haya yatufundisha ya kwamba kipawa cha Roho Mtakatifu cha kupita kawaida hutolewa kwa kuweka mikono na kuomba. Na kwa kuwa kipawa hiki hutoka kwa Mungu tu, sisi tulio hapa tumwombe Mwenyezi Mungu kwamba wao waliofanywa watoto wake katika Ubatizo awatie nguvu kwa Roho wake Mtakatifu katika kuthubutishwa.
Basi ninyi, mtakaowekewa mikono sasa, imewapasa kusema mbele ya mkutano huu kwamba mwakusudia sana kwa msaada wa kipawa hiki, kwenenda katika imani ya Kristo, na kutii mapenzi ya Mungu na amri zake; na kukiri waziwazi ya kwamba hamna budi kutimiza mambo ya Kikristo mliofungiwa na Ubatizo wenu.
|
Optional introduction (addition to 1662) |
¶ Hapo ndipo yule Bishopu hunena,
JE, ninyi mliopo mbele zake Mwenyezi Mungu, na mkutano huu, mwarejeza upya ile nadhiri yenye maana makuu, ile ahadi yenu iliyowekwa kwa majina yenu katika kubatizwa kwenu; huku mkikubali kuithubutisha ninyi wenyewe, na kuyakiri kuwa yamewalazimu kuyaamini na kuyatenda yote, madhamini wenu waliyojitweka wakati ule kwa ajili yenu?
¶ Ndipo wao hujibu kila mmoja, kwa sauti yenye kusikilikana,
Naam, ndiyo
¶ Ndipo yule Bishopu hunena,
MSAADA wetu u katika jina la Yehova,
Huitika. Aliyeumba mbingu na nchi.
Bishopu. Jina la Yehova na libarikiwe,
Huitika. Tokea sasa hata milele.
Bishopu. Ewe Bwana, utusikize maombi yetu,
Huitika. Kilio chetu kikufikilie uliko.
Bishopu
Na tuombe
EWE Mwenyezi Mungu, wewe una nguvu zote, nawe maisha yako ni ya milele, wewe umeridhika hata umewapa kuzawa upya hawa watumishi wako kwa maji na Roho Mtakatifu, umewapa na msamaha wa madhambi yao, pia yote; sisi twakuomba Bwana, uwatie nguvu watu hawa, kwa yule Msaada, yule Roho Mtakatifu; nawe kila siku uvikuze ndani yao vipawa vyako namna nyingi vya neema: navyo ni roho ya hekima na fahamu, roho ya shauri na nguvu za rohoni, roho ya maarifa na ya kumtii Mwenyezi Mungu kweli; nawe uwajalize roho yenye kukucha kwa utakatifu, sasa na hata milele. Amina.
¶ Ndipo hapo wao huja kwa taratibu yao na kupiga magoti kila mmoja mbele ya Bishopu, naye huwawekea mikono yake kadiri ya waliopo mmoja mmoja, akinena,
|
|
UMKINGE huyu mtoto wako, ewe Bwana, (au, Umkinge huyu mtumishi wako, ewe Bwana) kwa neema yako ya mbinguni, ili apate kudumu katika kuwa mtu wako milele, ili naye aongee kila siku katika Roho wako Mtakatifu, aendelee na mbele, hata aufikilie ufalme wako usio mwisho. Amina.
¶ Hapo ndipo yule Bishopu hunena,
BWANA na awe pamoja nanyi.
Huitika. Na awe pamoja na roho yako.
¶ Hata wakiisha kupiga magoti yule Bishopu huongeza kunena,
Na tuombe
|
The Confirmation |
BABAETU uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako na uje, Mapenzi yako yatendeke juu ya nchi, Kama yatendekavyo mbinguni. Utupe leo' mkate wetu wa kututosha. Nawe utusamehe makosa yetu, Kama nasi tulivyowasamehe watukosao. Nawe usitupeleke katika kujaribiwa, Utuokoe maovuni. Amina.
Na sala hii,
EWE Mwenyezi Mungu, una nguvu zote, na maisha yako ni ya milele; wewe ndiwe utupaye kuyapenda na kuyatenda ambayo ni ya kufaa na kupendekeza mbele zako, ewe Mungu Mfalme wetu; sisi tu miguuni pako, twawaombea hawa watumishi wako, ambao tumewawekea mikono sasa kwa kufuata. kielelezo cha mitume wako watakatifu, ili kuwapa hakika, kwa ishara hiyo, ya fadhili yako uliyo nayo kwao, na wema wako wenye neema. Nasi twakuomba sana, mkono wako wewe wa ubaba na uwe juu yao daima; Roho wako Mtakatifu naye awe pamoja nao milele, hata kwa jinsi utakavyowaongoza katika kulijua na kulitii Neno lako, iwe wao, mwisho wa yote, kuupata uzima wa: milele; kwa Bwana wetu Yesu Kristo, naye ndiye aishiye na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, uli Mungu mmoja daima, milele. Amina.
EWE Bwana Mweza, Mungu usiye mwanzo wala mwisho, twakuomba sana utuneemeshe ya kwamba mioyo yetu pamoja na miili yetu, vipate kuongozwa hivyo na kutakaswa na kutawaliwa na wewe, katika njia za sheria yako na vitendo vya mausio yako, ili, kwa vile utakavyotulinda duniani na ahera, tuhifadhike miili yetu na roho zetu; kwa Bwana wetu Mwokozi wetu Yesu Kristo. Amina.
¶ Ndipo hapo yule Bishopu huwaombea baraka, kwa kusema hivi:
BARAKA yake Mungu Mweza-wa-yote, Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, iwe juu yenu na kukaa kwenu milele. Amina.
|
Lord's Prayer |
Au hivi,
ENENDENI ulimwenguni na amani; muwe hodari; lishikeni lililo jema; msimlipe mtu mabaya kwa mabaya; watieni moyo walio wanyonge; wategemezeni wasio na nguvu; wasaidieni walio mashakani; waheshimuni watu wote; mpendeni Bwana na kumtumikia, mkifurahi katika nguvu za Roho Mtakatifu.
Na baraka ya Mwenyezi Mungu, Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, iwe mwenu ikae kwenu daima. Amina.
|
Optional blessing (addition to 1662) |
¶ Wala mtu asikaribishwe katika Ushirika Mtakatifu hata atakapowekewa mikono au kuwa mtu aliye tayari kwa kuwekewa mikono, naye yuataka kama hayo mwenyewe. |
|